DC ATAKA UBORA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO

Na, Ernest Magashi

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Mhandisi Paskasi Mragili, amewataka wakandarasi kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kupata ubora unaotarajiwa.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo iliyofanyika Machi 18, 2026, Mragili alisisitiza kuwa ni muhimu miradi yote kutekelezwa kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu ili kuongeza ufanisi na kudumu kwa muda mrefu.
Alieleza kuwa ziara hiyo ililenga kukagua miradi katika kata za Busonzo na Uyovu, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ubora unaokidhi viwango vilivyowekwa ili kuleta tija kwa wananchi.

“Tunachotaka kuona siyo tu miradi kukamilika, bali ikamilike kwa ubora uliokusudiwa na iendane na thamani ya fedha iliyotumika ili iweze kudumu kwa muda mrefu,” alisema Mragili.
Katika hatua nyingine, aliwataka wataalamu na wasimamizi wa miradi kufuatilia kwa karibu kila hatua ya utekelezaji ili kuepusha makosa yanayoweza kusababisha hasara au ucheleweshaji wa miradi.

Aidha, alihimiza ushirikishwaji wa wananchi katika kuchangia nguvu kazi kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wake.
Katika ziara hiyo, Mragili alikagua miradi mbalimbali ikiwemo ukamilishaji wa zahanati ya Busonzo, ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Msingi Nampalahala, pamoja na ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Kabagole.
Miradi mingine ni ukarabati wa vyumba tisa vya madarasa na ofisi moja ya walimu katika Shule ya Msingi Buganzu, ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na vyoo vyenye matundu sita katika Shule ya Msingi Kabuhima, pamoja na ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami nyepesi yenye urefu wa kilomita 1.2 katika eneo la Ibamba.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya aliambatana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, wajumbe wa Kamati ya Usalama pamoja na wataalamu mbalimbali wa halmashauri.
Akizungumza, Kagoma alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa mchango wake katika kuhamasisha maendeleo na kuwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Pia aliwataka wananchi kuendelea kujitolea kwa kuchangia nguvu kazi, ikiwemo kusogeza mchanga, mawe na maji ili kukamilisha miradi hiyo kwa wakati. 
Aliongeza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hivyo wananchi wanapaswa kuunga mkono jitihada hizo kwa vitendo.

Comments