Afisa Mnadhimu na Utawala (ACP) Adamu A. Maro wa Mkoa wa Geita amefungua rasmi mafunzo ya waandishi wa habari mkoani humo yanayolenga kuwajengea uwezo wa kuhakiki taarifa kwa kutumia mifumo ya Akili Unde (AI), akisisitiza umuhimu wa teknolojia hiyo katika kuboresha ubora wa habari zinazowasilishwa kwa umma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, ACP Maro alisema kuwa katika dunia ya sasa ya kidijitali, kasi ya usambazaji wa taarifa imeongezeka kwa kiwango kikubwa, hali inayochochea pia kuenea kwa taarifa potofu. Kutokana na changamoto hiyo, aliwataka waandishi wa habari kutumia zana za kisasa, ikiwemo teknolojia ya AI, ili kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi, zilizothibitishwa na zenye kuaminika.
Aliongeza kuwa taaluma ya uandishi wa habari inahitaji weledi wa hali ya juu pamoja na uadilifu, akiwahimiza waandishi kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuripoti habari. Aidha, aliwataka kuzingatia misingi ya ukweli, usahihi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Ni muhimu kwa waandishi wa habari kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ili kukabiliana na changamoto za upotoshaji wa taarifa. Matumizi sahihi ya AI yanaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha ukweli wa habari unalindwa,” alisisitiza ACP Maro.
Aidha, alisema Serikali pamoja na vyombo vya usalama vinatambua mchango mkubwa wa waandishi wa habari katika kuhabarisha umma na kulinda amani ya nchi. Hivyo, alieleza kuwa kuna umuhimu wa kuendelea kuwajengea uwezo na kuwawezesha kufanya kazi zao katika mazingira bora zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa Geita Press Club (GPC), Devid Azaria, alisema elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha utendaji wao, hususani katika kupambana na taarifa za upotoshaji. Waliahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, umakini na kuzingatia maadili ya taaluma yao kwa manufaa ya jamii.
Naye Mwenyekiti wa Geita Press Club (GPC), Renatus Masuguliko, alimshukuru mgeni rasmi pamoja na mwezeshaji wa mafunzo hayo, akieleza kuwa mafunzo hayo ya siku moja yamefadhiliwa na GPC kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi zaidi.

Comments
Post a Comment