Serikali imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 70 kupitia tozo, ada na ushuru mbalimbali zinazotokana na utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), na inatarajia mapato hayo kuongezeka hadi zaidi ya shilingi trilioni 2.3 mara mradi utakapoanza rasmi hatua ya uendeshaji.
Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, Februari 16, 2026 wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba katika mradi wa East African Crude Oil Pipeline (EACOP) mkoani Tanga.
Akizungumza katika ziara hiyo, Makamba amesema mradi huo umefikia asilimia 81 ya utekelezaji tangu ulipoanza mwaka 2022. Mradi unahusisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilomita 1,443, pamoja na miundombinu mingine ikiwemo matenki ya kuhifadhia mafuta na gati la kupakia mafuta katika pwani ya Tanga.
Amefafanua kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 5.649, ambapo Serikali ya Tanzania inachangia dola milioni 374, sawa na asilimia 15 ya hisa.
Kwa upande wa ajira, Makamba amesema mradi umewezesha ajira 10,000 katika kipindi cha ujenzi. Kati ya hizo, asilimia 75 sawa na ajira 7,500 zimenufaisha Watanzania wenye ujuzi wa chini na wa kati, huku asilimia 25 sawa na ajira 2,500 zikinufaisha wataalamu wa Kitanzania katika sekta za uhandisi, mitambo ya umeme, mazingira na taaluma nyinginezo.
Aidha, zaidi ya kampuni 200 za Kitanzania zimepata zabuni za kutoa huduma na bidhaa zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.325. Vilevile, barabara zenye urefu wa kilomita 304 zimeboreshwa ili kurahisisha shughuli za ujenzi na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi katika maeneo yanayopitiwa na mradi.
Makamba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa maono na msukumo wake katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio, akieleza kuwa juhudi zinazoendelea zitaiwezesha EACOP kukamilika ifikapo Julai 2026.

Comments
Post a Comment