Watu wenye ulemavu wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi katika mgodi wa dhahabu wa Msasa (Msasa Gold Mine), uliopo Kata ya Runzewe Magharibi, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameupongeza uongozi wa mgodi huo kwa kuendelea kuwajali na kuwaunganisha na wachimbaji ili wanufaike na mgao wa mawe yenye dhahabu.
Wakizungumza katika eneo maalum walilotengewa kwa ajili ya kukusanyia mawe wanayopewa, mmoja wa watu wenye ulemavu wa viungo, Doricas Samson, alisema uongozi wa mgodi umekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kundi hilo haliachwi nyuma. Alieleza kuwa mara baada ya wachimbaji kupata mawe, watu wenye ulemavu hupewa fursa ya kuchukua kiasi kidogo cha mawe, kuyasaga na kuyakamua dhahabu, jambo linalowasaidia kupata kipato cha kujikimu kimaisha.
Doricas alisema awali kipato chake kilikuwa kati ya shilingi 5,000 hadi 10,000 kwa siku, lakini kwa sasa kimeongezeka hadi kufikia shilingi 30,000 kwa siku, hali inayomwezesha kugharamia mahitaji ya familia yake na kuwasomesha watoto wake.
Alibainisha kuwa miongoni mwa watu wenye ulemavu waliopo mgodini hapo wapo waliopooza, wengine wanaotembea kwa kutumia magongo au kujivuta kwa mikono, huku mazingira ya mashimo (maduara) yakiwa na changamoto ya usalama. Kutokana na hali hiyo, aliomba uongozi wa mgodi kuweka utaratibu maalum wa kuwapatia gawio lao bila kulazimika kufika karibu na maduara, ili kuwalinda dhidi ya hatari ya kuanguka.
Kwa upande wake, Thomas Masubo, naye ni mtu mwenye ulemavu, aliipongeza idara ya ukaguzi na usalama ya mgodi huo kwa kuhakikisha usalama wa watu wenye ulemavu wanapopita katika maeneo ya uchimbaji. Alisema kupitia utaratibu uliopo, kipato chake kimeongezeka kutoka shilingi 1,000 hadi kufikia shilingi 10,000 kwa siku.
Masubo aliwahimiza wachimbaji kuacha migogoro isiyo ya lazima na uongozi wa mgodi ili manufaa ya mgodi yaweze kuwafikia watu wote, hususan makundi yenye mahitaji maalum. Aliongeza kuwa hajawahi kushuhudia ubaguzi wowote dhidi ya watu wenye ulemavu, kwani uongozi wa mgodi na idara ya usalama umekuwa ukihakikisha haki na usalama wao.
Akizungumza kwa niaba ya idara ya ukaguzi na usalama, Mkuu wa Idara hiyo katika Mgodi wa Msasa Gold Mine, Chief James Nkamba maarufu kama G’wanankamba, alisema usalama mgodini ni wa kipaumbele kikubwa. Alifafanua kuwa mgodi una zaidi ya maduara 700 yanayoendelea kuchimbwa, hivyo idara yake imejipanga kuhakikisha usalama kwa wachimbaji wote wakiwemo watu wenye ulemavu.
Chief Nkamba alisema idara yake inaendelea kuimarisha usalama kwa kushirikiana na Serikali kupitia wahandisi kutoka Ofisi ya Madini Kanda ya Mbogwe, ambao wamekuwa wakitoa elimu na maelekezo ya kiusalama kwa wachimbaji. Alisisitiza kuwa askari wa ukaguzi wapo muda wote kuhakikisha kanuni za usalama zinafuatwa masaa 24.Aidha, aliwashukuru wachimbaji kwa kuzingatia maelekezo ya usalama, hatua iliyosaidia kuufanya mgodi huo kuwa salama zaidi.
Naye Meneja wa Mgodi wa Msasa Gold Mine, Kessy Maira, alisema uongozi wa mgodi unatambua mchango na uwepo wa watu wenye ulemavu, hivyo umeweka utaratibu wa kuwapa kiasi cha mawe ya dhahabu ili waweze kujipatia kipato na kuboresha maisha yao kiuchumi.Aliongeza kuwa mgodi huo umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wananchi, ambapo baadhi wamefanikiwa kujenga nyumba bora, kununua magari na kuendesha shughuli mbalimbali za maendeleo. Meneja huyo pia aliipongeza Serikali ya Kijiji cha Msasa kwa ushirikiano mzuri.
Hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Mragili, aliwataka wachimbaji katika eneo hilo kufuata taratibu zilizowekwa na uongozi wa mgodi, kuepuka migogoro na kuhakikisha wanazingatia kikamilifu masuala ya usalama, akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kusimamia ulinzi wa maisha ya wananchi.

Comments
Post a Comment