WANANCHI WAUNGANA NA DKT. BITEKO KUISHUKURU SERIKALI KWA GARI LA ZIMAMOTO BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

Wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wameungana na Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia wilaya hiyo gari la Zimamoto na Uokoaji kwa ajili ya kukabiliana na majanga ya moto.Wananchi hao wamesema ujio wa gari hilo utaondoa hofu iliyokuwepo kwa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa huduma ya haraka ya zimamoto pindi majanga yanapotokea, hali iliyokuwa ikisababisha hasara kubwa kwa mali na wakati mwingine maisha ya watu.Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Thomas James alisema serikali imefanya jambo muhimu na la kihistoria kwa wakazi wa Bukombe, kwani sasa wana uhakika wa uwepo wa kikosi cha zimamoto chenye vifaa vya kisasa kwa ajili ya uokoaji na kuzima moto.Naye Mariet Paul alimpongeza Dkt. Biteko kwa juhudi zake za kuendelea kuleta maendeleo wilayani humo kwa kushirikiana na serikali. Alisema tangu kuanzishwa kwa wilaya hiyo, hiyo ni mara ya kwanza kupatikana kwa gari la zimamoto, jambo linalodhihirisha dhamira ya kweli ya kuboresha huduma za dharura kwa wananchi.Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, akikabidhi rasmi gari hilo, alisema uwepo wa gari la Zimamoto na Uokoaji katika halmashauri hiyo utaongeza kasi na ufanisi katika kukabiliana na majanga ya moto pamoja na shughuli za uokoaji.Alisisitiza kuwa ujio wa gari hilo ni suluhisho la kudumu kwa changamoto ya matukio ya moto yaliyokuwa yakisababisha hasara kubwa kwa wananchi na wafanyabiashara. 

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuimarisha huduma za dharura ili kuhakikisha usalama wa maisha na mali za wananchi unalindwa wakati wote.Aidha, aliwataka askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kulitunza gari hilo kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji ili liweze kutoa huduma bora kwa jamii na kufika kwa wakati katika maeneo ya matukio.Kwa upande wake, Dkt. Biteko aliishukuru serikali kwa kuipatia Bukombe gari hilo na kuwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, hasa wakati wa majanga, ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi.Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Mragili, aliishukuru serikali kwa msaada huo na kuahidi kuwa gari hilo litatunzwa vizuri na kuhakikisha linafanya kazi kama ilivyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi wote.

Ujio wa gari hilo ni hatua muhimu katika kuimarisha miundombinu ya huduma za dharura na kuifanya Bukombe kuwa salama zaidi dhidi ya majanga ya moto.

Comments