WACHIMBAJI WAIPONGEZA SERIKALI KUSOGEZA SOKO LA DHAHABU MSASA


Na, Ernest Magashi

Wachimbaji wa dogo wa madini ya dhahabu katika Mgodi wa Msasa Gold Mine, uliopo Kijiji cha Msasa, Kata ya Runzewe Magharibi, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuwasogezea soko la dhahabu karibu na eneo la mgodi, hatua ambayo imewaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji, Meneja wa Mgodi wa Msasa Gold Mine, Kessy Maira, alisema uwepo wa soko la dhahabu ndani ya mgodi umeimarisha udhibiti wa madini na kupunguza kwa kiasi kikubwa vitendo vya bazi ya wachimbaji kusafiri na dhahabu.Meneja Maira alisema uongozi wa mgodi kwa kushirikiana na maafisa wa Tume ya Madini umekuwa ukiwahamasisha wachimbaji kuhakikisha kuwa baada ya kumaliza kusaga na kuchambua dhahabu, wanakwenda kuuza kwenye soko rasmi la dhahabu la Msasa badala ya kusafiri na dhahabu kwenda maeneo ya mbali.“Naipongeza Serikali kwa kusogeza huduma ya soko la dhahabu kwa wachimbaji waliopo Mgodi wa Msasa Gold Mine. Hatua hii imeleta mabadiliko makubwa kwani awali wachimbaji walilazimika kusafiri umbali mrefu hadi Ushirombo au Geita, lakini sasa wanauzia hapa hapa Msasa,” alisema Meneja Maira.Aliongeza kuwa kuwepo kwa soko hilo kumeimarisha usalama mgodini na kuvutia wananchi wengi zaidi kutafuta fursa za kiuchumi. Alisema shughuli za mgodi zimenufaisha makundi mbalimbali yakiwemo mama lishe, wachota maji, waendesha bodaboda, machinga na wafanyabiashara wengine, ambao wamekuwa wakitumia fursa hiyo kukuza uchumi wao.Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Ukaguzi na Usalama wa Mgodi wa Msasa Gold Mine, Chief James Nkamba maarufu kama Ng’wanankamba, alisema idara yake imejipanga kuhakikisha usalama katika maduara wakati wote, iwe ni wakati wa jua au mvua, ili wachimbaji waendelee na uzalishaji bila kuhatarisha maisha yao.Chief Nkamba aliwaomba wachimbaji kuendelea kuzingatia maelekezo ya askari wa idara ya ukaguzi na kushiriki kikamilifu katika masuala ya usalama.Miongoni mwa wachimbaji wa mgodi huo, Balele Musa aliipongeza Serikali na uongozi wa mgodi kwa kushirikiana kutoa vibali halali vya uchimbaji na kuhakikisha usalama katika maduara na maeneo mengine ya mgodi. Alisema shughuli za uchimbaji zinaendelea vizuri na zimewawezesha wachimbaji kujipatia kipato, kuwasomesha watoto na kujenga makazi bora.Naye Adelina Renatusi, akizungumza kwa niaba ya wanawake wachimbaji, alisema mgodi wa Msasa umechangia kuongeza kipato cha wanawake na kuwawezesha kushiriki katika majukumu ya kifamilia, ikiwemo kuwasomesha watoto kwa kushirikiana na waume zao.Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mabroker wa Dhahabu Tanzania, Bahati Makai, alipokuwa kwenye soko la dhahabu la Mgodi wa Msasa Gold Mine, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha wachimbaji kufanya kazi kwa uhuru bila usumbufu.Aidha, Makai alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa mchango wake wakati akiwa Waziri wa Madini, akieleza kuwa alisaidia kuanzishwa kwa Chama cha Mabroker wa Dhahabu Tanzania, hatua iliyosaidia kuboresha hadhi na mazingira ya kazi ya mabroker nchini.“Namshukuru sana Dkt. Doto Biteko kwa kusaidia kuanzishwa kwa chama cha mabroker. Kabla ya hatua hiyo, mabroker licha ya kuwa na leseni halali walionekana kama watu wasioaminika, lakini sasa wanafanya kazi kwa uhuru na kwa kushirikiana na maafisa wa madini kila mkoa,” alisema Makai.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mabroker wa Dhahabu Tanzania, Jeremia Simon, alimpongeza Afisa Madini wa Mkoa wa Kimadini Mbogwe kwa kutenga eneo maalum la ofisi ya soko la dhahabu ndani ya Mgodi wa Msasa Gold Mine, jambo lililowapunguzia wachimbaji gharama na usumbufu wa kusafiri umbali mrefu.Simon aliipongeza Serikali kupitia Tume ya Madini na Wizara ya Madini kwa kuendelea kushirikiana na uongozi wa mgodi katika kuimarisha ulinzi na usalama, akibainisha kuwa mgodi huo una zaidi ya watu 50,000 wanaojishughulisha na shughuli za uzalishaji mali, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.Hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Mragili, alitoa wito kwa wachimbaji kuenkdelea kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu na masharti ya mmiliki wa leseni pamoja na kanuni za usalama, akisisitiza kuwa usalama wa wachimbaji ni kipaumbele cha Serikali.

Comments