VITENGO VYA UFUATILIAJI NA TATHMINI WIZARA YA MAJI NA NISHATI KUUNGANISHA NGUVU KUSIMAMIA MIRADI


Na, Ernest Magashi

Vitengo vya Ufuatiliaji na Tathmini vya Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati vimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi, kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wenye ufanisi na kuwanufaisha wananchi kupitia huduma bora za maji na nishati.Makubaliano hayo yamefikiwa leo katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Maji, Mtumba jijini Dodoma, kikihusisha wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini kutoka wizara zote mbili.Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Nishati, Anitha Ishengoma, amesema vitengo vya ufuatiliaji na tathmini vina jukumu muhimu la kuhakikisha sera, mipango na miradi ya wizara pamoja na taasisi zake zinatekelezwa kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.“Ni muhimu kwa vitengo vya ufuatiliaji na tathmini kuhakikisha sera na mipango ya wizara na taasisi zake inatekelezwa ipasavyo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za maji na nishati kwa wananchi,” amesema Ishengoma.Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Maji, Diana Kimario, amesema wizara hizo zimekuwa zikishirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayogusa sekta zote mbili.Ametolea mfano Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (MW 2,115), akieleza kuwa kuimarisha ushirikiano kati ya wizara hizo kutachochea matokeo chanya zaidi katika usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Comments