TAASISI 1,136 ZAHAMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KATI YA 30,000 NCHINI

Na, Ernest Magashi

Wizara ya Nishati imesema kuwa hadi sasa jumla ya taasisi 1,136 kati ya taasisi 30,000 zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku nchini, zimefanikiwa kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni hatua muhimu katika jitihada za kitaifa za kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa.Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 3, 2026 na Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Nolasco Mlay, wakati wa uzinduzi wa mtambo wa gesi ya kupikia (LPG Vaporizer) katika Shule ya Sekondari Azania jijini Dar es Salaam.Amesema mtambo huo umejengwa kwa ushirikiano kati ya KAGLA Eco Friendly na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi za umma, hususan shule.Mlay amebainisha kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ajenda ya kimkakati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara wa kampeni hiyo si tu nchini bali pia barani Afrika.

Amesema licha ya hatua zilizofikiwa, bado kuna kazi kubwa ya kufanywa kutokana na idadi kubwa ya taasisi zinazohitaji kuhamia kwenye nishati safi.

“Kati ya taasisi 30,000 zinazolisha watu zaidi ya 100 nchini, ni taasisi 1,136 pekee ndizo zilizohamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia. Hivyo, ushiriki wa wadau ni muhimu ili kufikia lengo la kitaifa la kuachana kabisa na matumizi ya mkaa na kuni,” amesema Mlay.

Ameongeza kuwa mchango wa wadau binafsi na wa kimataifa, akitolea mfano KAGLA Eco Friendly, ni nguzo muhimu katika kufanikisha azma ya Serikali ya kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Azania, Melsius Kayombo, amesema shule hiyo yenye wanafunzi 300 itanufaika kwa kiasi kikubwa na mradi huo, hususan katika kurahisisha upishi na kuboresha ratiba za masomo.“Tumekuwa tukiusubiri mradi huu tangu mwaka 2024. Kukamilika kwake kutapunguza muda wa maandalizi ya chakula, kulinda afya za wapishi na kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula kwa wakati ili kuendelea na masomo yao bila usumbufu,” amesema Kayombo.Naye, Mtaalamu kutoka KAGLA Eco Friendly na mfadhili wa mradi huo, Hiroyuki Shimada, amesema teknolojia ya LPG Vaporizer iliyowekwa katika shule hiyo ni salama, ya kisasa na ya kipekee, ikiwa ni ya kwanza kutumika nchini Tanzania.

Ameeleza kuwa mfumo huo una uwezo wa kutoa taarifa za moja kwa moja kuhusu ufanisi na usalama wa mtambo, hatua itakayosaidia taasisi kudhibiti matumizi na kupunguza gharama za nishati ya kupikia.


Comments