Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa shilingi bilioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kusambaza Umeme cha Imalilo kilichopo Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, mradi unaotarajiwa kukamilika Mei 2026.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya umeme mkoani Simiyu, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, alisema mradi huo utagharimiwa kwa asilimia 100 na Serikali na unalenga kuimarisha ubora na upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Bariadi na maeneo ya jirani.
Twange alisema miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kusambaza Umeme cha Imalilo pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 220 (220kV) kutoka Shinyanga hadi Simiyu.
Alifafanua kuwa mradi wa Kituo cha Imalilo ulianza kutekelezwa mwezi Oktoba 2025 kwa kutumia wataalamu wa ndani wa TANESCO na unatarajiwa kukamilika Mei 2026.
“Baada ya muda mrefu, tumeanza kutekeleza mradi huu kupitia wataalamu wetu wa ndani tangu Oktoba 2025, na tunatarajia kuukamilisha Mei 2026,” alisema Twange.
Kwa sasa, wananchi wa Bariadi wanategemea umeme unaosambazwa kutoka mikoa ya Shinyanga, Mwanza na Mara, hali inayosababisha kupungua kwa ubora wa umeme kutokana na umbali mrefu wa kusafirisha nishati hiyo.
Kwa mujibu wa Twange, kukamilika kwa Kituo cha Imalilo kutaondoa changamoto hiyo kwa kuimarisha miundombinu ya umeme na kuongeza uthabiti wa huduma, hivyo wananchi wa Bariadi na maeneo ya jirani wanatarajiwa kupata umeme wa uhakika kuanzia Juni 2026.
“Ujenzi wa kituo hiki utaimarisha miundombinu ya umeme na kuondoa changamoto za kushuka kwa ubora wa huduma. Kuanzia Juni 2026, wananchi watapata umeme wa uhakika zaidi,” aliongeza.
Kwa sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 20.75. Mradi unagharimu shilingi bilioni 8, fedha zinazofadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wake.

Comments
Post a Comment