Serikali imezitaka taasisi na wadau wa sekta ya fedha nchini kubuni na kutoa huduma pamoja na bidhaa za kifedha zitakazochochea na kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususani kwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo waliopo maeneo ya pembezoni na vijijini pamoja na wabunifu wa teknolojia za nishati hiyo.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, leo Februari 4,2026, wakati akimwakilisha Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, katika uzinduzi wa mradi wa nishati safi ya kupikia uliofanyika katika Shule ya Sekondari Bunge Wasichana, mkoani Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Salome amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, ambapo matumizi ya nishati hiyo yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 23.2 mwaka 2025.
“Hata hivyo, bado takribani asilimia 77 ya kaya nchini zinaendelea kutumia nishati isiyo safi ya kupikia. Hivyo, naendelea kuwasihi wadau wa sekta binafsi na sekta ya fedha kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kusukuma mbele ajenda hii kwa kuwezesha upatikanaji wa nishati safi, hasa katika maeneo ya vijijini na pembezoni,” amesema Salome.
Aidha, Naibu Waziri huyo amewataka wasambazaji wa gesi ya kupikia kuongeza vituo vya usambazaji na ujazaji wa mitungi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi wengi zaidi. Pia amewahimiza vijana na wabunifu waliopo vyuoni kuendelea kufanya tafiti na kubuni teknolojia bunifu zitakazosaidia kueneza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Akizungumzia mradi aliouzindua, Salome amesema kuwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali linalozitaka taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa siku kutumia nishati safi ya kupikia, kwa lengo la kulinda afya za binadamu na mazingira.
Ameongeza kuwa mfumo huo wa nishati safi uliowekwa shuleni hapo utawezesha upishi wa chakula kwa usafi, kwa haraka, kwa ufanisi na kwa gharama nafuu, huku ukiwaondolea wapishi na wanafunzi madhara yatokanayo na moshi, na hivyo kuchangia pia uhifadhi wa mazingira.
Naibu Waziri Salome ameeleza kuwa uzinduzi wa mradi huo ni sehemu ya jitihada za kitaifa zinazoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Hadi sasa, tayari asilimia 23.2 ya wananchi wamehamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku taasisi 1,136 zinazohudumia zaidi ya watu 100 kwa siku zikiwa tayari zimebadilisha mifumo yao ya nishati.
Katika hafla hiyo, Salome alizindua pia Klabu ya Nishati Safi ya Kupikia (Clean Cooking School Club) katika Shule ya Sekondari Bunge Wasichana, ambayo ni klabu ya kwanza ya aina yake nchini Tanzania. Klabu hiyo inatarajiwa kuwa mfano wa kuigwa na shule nyingine nchini katika kueneza elimu ya nishati safi ya kupikia.
Wanafunzi watakaokuwa wanachama wa klabu hiyo watatambuliwa kama Vinara wa Nishati Safi ya Kupikia (Clean Cooking Champions), na watashirikiana na Wizara ya Nishati pamoja na wadau mbalimbali katika kutoa elimu mashuleni na kwenye jamii, sambamba na kubuni teknolojia rafiki kwa afya na mazingira.
Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bunge Wasichana, Richard Msana, amesema shule hiyo yenye wanafunzi 555 imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za nishati ya kupikia baada ya kuachana na matumizi ya kuni na kuhamia matumizi ya gesi.
Msana amesema kuwa kati ya Julai 2020 hadi Mei 2022, shule ilikuwa ikitumia takribani shilingi milioni 10.5 kila baada ya miezi mitatu kununua kuni. Baadaye, ilipoanza kutumia mkaa mbadala, gharama zilipungua hadi kufikia shilingi milioni 2.7.
Ameongeza kuwa kwa sasa, kupitia mradi wa matumizi ya gesi, shule hununua tani moja ya gesi inayotumika kwa kipindi cha miezi miwili, ambapo wastani wa gharama ni shilingi milioni 1.3 kwa mwezi, kiwango ambacho ni nafuu zaidi kiuchumi na rafiki kwa mazingira.

Comments
Post a Comment