Rais wa Zanzibr na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amepongeza wazo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kujenga Chuo cha Mafunzo ya Diplomasia na Huduma za Bunge Zanzibar, akisema hatua hiyo itaongeza hadhi ya visiwa hivyo katika ramani ya kimataifa ya elimu ya juu.
Rais Dkt. Mwinyi aliyasema hayo leo, Februari 18, 2026, alipokutana na wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Bunge wakiongozwa na Spika wa Bunge hilo, Mussa Azan Zungu, waliofika Ikulu, Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi alisema Zanzibar inahitaji kuwa na vyuo vikuu zaidi vitakavyotoa mafunzo ya viwango vya juu katika fani mbalimbali, hatua itakayoiwezesha kuwa kitovu cha elimu na tafiti katika ukanda wa Afrika Mashariki na kimataifa.
Alieleza kuwa ujenzi wa chuo hicho ni fursa adhimu kwa taifa, kwani utavutia wanafunzi na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali, jambo litakalochochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya elimu na huduma zinazohusiana nayo, ikiwemo utalii wa kielimu.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi aliwahakikishia wajumbe hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo, na kuwataka kuharakisha mchakato wa kuufanikisha ili Zanzibar iweze kunufaika na fursa hiyo mapema.
Kwa upande wake, Spika Mussa Zungu alimpongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa uongozi wake thabiti ulioleta mageuzi makubwa ya maendeleo Zanzibar, hususan katika ujenzi wa miundombinu ya barabara na kasi ya ukuaji wa uchumi unaokwenda sambamba na mabadiliko ya dunia.
Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Bunge wako Zanzibar kwa ajili ya mafunzo ya siku tatu ya uongozi kwa Kamati ya Uongozi na Tume ya Utumishi ya Bunge, yaliyofanyika Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Comments
Post a Comment