Bukombe, Geita
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukombe, Matondo Kihanda Lutonja, ameanza rasmi ziara ya kutembelea matawi ya chama katika kata mbalimbali za wilaya hiyo kwa lengo la kukagua uhai wa chama, kuimarisha uongozi wa mashina na matawi pamoja na kusikiliza changamoto za wanachama.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti Lutonja amefungua matawi mapya matatu ikiwa ni sehemu ya jumla ya matawi zaidi ya 80 mapya yaliyoanzishwa katika Kata za Namonge, Busonzo na Uyovu. Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni mkakati mahsusi wa chama wa kusogeza huduma karibu na wanachama na kuongeza nguvu ya kisiasa katika ngazi ya msingi.
Akizungumza na wanachama, Mwenyekiti huyo alipongeza juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuleta na kutekeleza miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Bukombe. Alibainisha kuwa katika kipindi cha uongozi wake, wilaya hiyo imenufaika kwa kiasi kikubwa kupitia uwekezaji katika sekta za elimu, afya, miundombinu ya barabara, maji safi na salama pamoja na upatikanaji wa umeme vijijini.
Aidha, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Doto Biteko, kwa juhudi zake za kuipambania Bukombe na kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inatekelezwa kwa manufaa ya wananchi.
Ziara hiyo inatarajiwa kuendelea katika kata nyingine za wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya chama kuelekea utekelezaji wa majukumu yake ya kisiasa na maendeleo ya jamii kwa ujumla. Wanachama wametakiwa kuendelea kushirikiana, kudumisha umoja na kukilinda chama ili kiendelee kuwa imara na chenye ushawishi katika ngazi zote.









Comments
Post a Comment