Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukombe Mkoa wa Geita, Daniel Lutonja, amewapongeza madiwani na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya CCM kupitia usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
Lutonja ametoa pongezi hizo katika kikao cha Baraza la Madiwani wakati wa uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutoka katika kata mbalimbali za wilaya hiyo.
Amesema kuwa viongozi wa CCM wanaposhuhudia miradi ikitekelezwa kwa usimamizi mzuri wa madiwani na wataalamu, hupata uhakika kuwa Ilani ya chama inatekelezwa ipasavyo kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi, ikiwemo ujenzi wa miundomibu za Afya na Elimu.
Aidha, Lutonja alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kuendelea kuwaunganisha wananchi, madiwani na wataalamu kwa lengo la kuijenga Bukombe kiuchumi na kijamii.
Awali, Dkt. Biteko aliwataka madiwani na wataalamu kuendeleza mshikamano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayopata fedha nyingi kutoka Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili miradi iliyokamilika na inayoendelea iweze kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alimuhakikishia Mwenyekiti wa CCM pamoja na Mbunge Dkt. Biteko kuwa wataendelea kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya madiwani na wataalamu, sambamba na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo.

Comments
Post a Comment