MSIBA WA ASKARI WA USALAMA BARABARANI WAACHA SIMANZI MWANZA


Na, Ernest Magashi

Jijini Mwanza kumeghubikwa na simanzi kufuatia kifo cha askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Koplo wa Polisi (CPL) Tumsifu Wilson Kileo (F7768), ambaye mwili wake umeagwa na mamia ya waombolezaji kabla ya kusafirishwa kwenda Lyamungo mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.Marehemu alifariki dunia baada ya kugongwa na daladala iliyopoteza mwelekeo wakati akiwa kazini akiongoza magari na kusimamia usalama barabarani. Ajali hiyo ilitokea Februari 10, 2026 majira ya saa 2:00 asubuhi katika mzunguko wa Mwanza Hotel katikati ya Jiji la Mwanza.Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Buhongwa, Lucas Baskely, aliyeongoza ibada ya kuuaga mwili wa marehemu, aliwataka madereva kuacha uzembe barabarani na kutotumia vyombo vya moto kama silaha ya kuhatarisha maisha ya wengine. Alisisitiza kuwa hakuna safari iliyo na thamani kuliko uhai wa binadamu.Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, alitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, akieleza kuwa CPL Tumsifu alikuwa askari mwenye nidhamu, weledi wakati wote kazini, ambaye Jeshi la Polisi bado lilikuwa linamuhitaji katika kulinda usalama wa raia na mali zao.Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Februari 16, 2026 aliongoza mamia ya maafisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali pamoja na wananchi katika kuuaga mwili wa marehemu. CPL Tumsifu alifariki dunia Februari 13, 2026 katika hospitali ya Rufaa Bugando alipokuwa akipatiwa matibabu.Akizungumza na waombolezaji, Mkuu huyo wa Mkoa aliwahimiza askari na wananchi kuenzi maisha ya marehemu kwa kuendeleza mema aliyoyaacha katika kulitumikia Jeshi la Polisi na jamii kwa ujumla.

Comments