Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa mchango wake wa vifaa vya ujenzi katika miradi ya maendeleo, wakieleza kuwa hatua hiyo ni kuendelea kuwashika mkono wananchi katika juhudi za kujiletea maendeleo.
Pongezi hizo zimetolewa na Diwani wa Kata ya Bukombe, Rozalia Masokola, wakati akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya kata hiyo katika kikao cha Baraza la Madiwani. Amesema Dkt. Biteko amechangia ujenzi wa Zahanati ya Itunga kwa kutoa mabati, mbao pamoja na kugharamia fundi, ambapo kwa sasa ujenzi umefikia hatua nzuri.
Naye Diwani wa Kata ya Runzewe Mashariki, Mery Nchiba, akiunga mkono hoja hiyo, amesema mchango wa mbunge huyo umeongeza hamasa kwa wananchi kujitolea nguvu kazi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye kata zao.
Katika hatua nyingine, Nchiba amelipongeza Baraza hilo pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, kwa kutenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha kuhifadhi maiti katika kituo cha afya, ili kupunguza adha wanayopata wananchi wanapofiwa na ndugu zao.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji Adelina Mfikwa amesema halmashauri itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa kushirikiana na madiwani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, aliwataka madiwani kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wataalamu ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wananchi. Pia alimpongeza Diwani wa kata ya Ng'anzo Masha Shig’wenda kwa usimamizi mzuri wa miradi katika kata yake, akibainisha kuwa katika baadhi ya miradi kumekuwa na fedha zinazobaki kutokana na matumizi sahihi.
Akijibu pongezi hizo, Dkt. Biteko aliwashukuru madiwani na kutumia Baraza hilo kuwataka kuendelea kusimamia kwa karibu miradi inayopata fedha kutoka Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, aliwasisitiza madiwani kuimarisha ushirikiano wao na wataalamu wa halmashauri ili kuhakikisha Bukombe inaendelea kupiga hatua za maendeleo endelevu.

Comments
Post a Comment