KUKAMILIKA KWA DARAJA LA BUGELENGA (MITA 60.54) KUFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI BUKOMBE NA MBOGWE


Na, Ernest Magashi

Kukamilika kwa Daraja la Bugelenga lenye urefu wa mita 60.54 kunatarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya za Bukombe na Mbogwe mkoani Geita, hasa katika kurahisisha usafirishaji wa mazao na mawasiliano kati ya wilaya hizo mbili.Akizungumza wakati wa kukagua daraja hilo, Diwani wa Kata ya Bugelenga, Donald Lubigisa, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, kwa kutekeleza ahadi yake ya kuhakikisha daraja hilo linajengwa na kukamilika kwa wakati.Lubigisa alisema mradi huo umegharimu Shilingi milioni 583.83 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia maombi yaliyowasilishwa na mbunge huyo baada ya kuombwa na diwani pamoja na wananchi.Alieleza kuwa daraja hilo linaunganisha moja kwa moja Wilaya ya Bukombe na Mbogwe, na limeondoa changamoto ya usafiri hasa kipindi cha masika, ambapo awali wananchi walipata shida kubwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni.“Ninamshukuru Mbunge Dkt. Biteko kwa kuwa msikivu na kufuatilia kwa karibu changamoto za wananchi. Pia nampongeza Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Msoka Msumba, kwa usimamizi mzuri wa mradi huu hadi kukamilika kwake,” alisema Lubigisa.Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Msoka Msumba, alisema ujenzi wa daraja hilo umekamilika kwa wakati kama ilivyopangwa, na kubainisha kuwa lenye urefu wa mita 60.54 ni miongoni mwa madaraja marefu ya mawe katika Mkoa wa Geita. Aliongeza kuwa mradi huo umegharimu jumla ya Shilingi milioni 583.83.Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Bugelenga walitoa shukrani kwa Serikali kwa kuboresha miundombinu hiyo, wakisema daraja hilo limekuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto za usafirishaji wa mazao, hasa wakati wa mvua kubwa.Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkange, Timbola Kasungwa, aliipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa daraja hilo limekuwa mhimili muhimu wa uchumi kwa vijiji vya mpakani, na linatarajiwa kuongeza kipato cha wananchi mmoja mmoja pamoja na taifa kwa ujumla.

Comments