KAMATI YA SIASA CCM (W) BUKOMBE YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO YENYE THAMANI ZAIDI YA BILIONI 30, KASI NA UBORA WARIDHISHA

 


Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukombe imekagua miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 30, ikieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji na ubora wa kazi zinazoendelea kutekelezwa wilayani humo.


Ziara hiyo iliyofanyika Februari 19, 2026, ilihusisha miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha huduma za kijamii na kukuza uchumi wa eneo hilo.


Miradi iliyotembelewa ni pamoja na:


Ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na makazi yake


Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe 



Barabara za lami zenye urefu wa kilometa 3.35 katika kata za Katente na Igulwa



Ujenzi wa madarasa katika Shule za Msingi Kakoyoyo na Businda




Mradi wa maji Kata ya Iyogelo Wenye thamani Zaidi ya Milioni 400 utakaowanufaisha wakazi wapatao 2,750





Katika mradi wa maji Iyogelo, kamati ilishuhudia huduma ya maji kutoka kwenye mabomba, hatua inayodhihirisha kukamilika kwa miundombinu muhimu na matarajio ya kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.


Soko Kuu na Stendi ya Kisasa




Wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Soko Kuu la Kisasa na Stendi ya Mabasi Ushirombo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Mhe. Erick Kagoma, alisisitiza usimamizi wa karibu kwa wakandarasi ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.


Aidha, aliwapongeza wakandarasi kutoka China kwa kasi na ubora wa kazi, huku akiahidi ushirikiano wa halmashauri katika kuhakikisha mazingira bora ya uwekezaji.


Pamoja na mafanikio hayo, ilielezwa kuwa wilaya inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa nguvu kazi kutokana na vijana wengi kuelekea kwenye shughuli za uchimbaji dhahabu. Hali hiyo hulazimu wakati mwingine kuajiri wafanyakazi kutoka nje ya wilaya.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukombe, Matondo Lutonja, alipongeza Kamati ya Siasa, wataalamu wa halmashauri na Baraza la Madiwani kwa usimamizi thabiti wa miradi, akisisitiza kuongeza kasi ya utekelezaji ili kukamilika kwa wakati.


Suala la magari makubwa kushusha mizigo sokoni pia lilijadiliwa. Ilielezwa kuwa mchakato wa kutenga eneo maalum kwa ajili ya malori yenye uzito wa zaidi ya tani 10 umeanza, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya eneo la Strabag (Runzewe) kwa matumizi hayo.


Ziara hiyo ilijumuisha viongozi wa Kamati ya Siasa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri, kwa lengo la kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta tija kwa wananchi wa Bukombe.

Comments