Na, Ernest Magashi
Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita imetenga shilingi milioni 70 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Igulwa, hatua itakayosaidia kupunguza adha kwa wananchi wanaolazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wakati wa kujadili hoja za Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bukombe, Adelina Mfikwa, alisema fedha hizo tayari zimepangwa kwenye bajeti na zitasafirishwa kwenye akaunti husika ili kuanza hatua za mwisho za ukamilishaji wa mradi huo.
Kauli hiyo ilitolewa kufuatia swali la Diwani wa Kata ya Igulwa, Richard Mabenga, aliyehoji ni lini zahanati hiyo itakamilika, akieleza kuwa wananchi wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu licha ya kuchangia nguvu na mali zao kuanzisha mradi huo kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko.
Diwani Mabenga alisema mradi huo ulianza mwaka 2018 kwa nguvu za wananchi walioweza kuchangia zaidi ya shilingi milioni nne, lakini ukakwama katika hatua ya renta.
“Naomba leo nipate majibu ya uhakika. Mradi huu umekuwa kero hata wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Kama fedha zipo, naomba utekelezaji uanze mara moja ili kumaliza changamoto hii,” alisema Mabenga.
Mwenyekiti wa Halmashauri, Erick Kagoma, alielekeza kuwa ifikapo robo ya tatu ya mwaka wa fedha, kiasi hicho cha shilingi milioni 70 kiwe kimepelekwa kwenye mradi huo ili ujenzi ukamilike na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadis Paskas Mragili, aliwapongeza madiwani na wataalamu kwa ushirikiano wao katika kutenga bajeti kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi moja kwa moja.
Aidha, aliwataka madiwani kuhamasisha wazazi na walezi kuwapeleka watoto waliofikia umri wa kuandikishwa shuleni kuanza darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza kwa wakati, ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha sekta ya elimu kupitia sera ya elimu bila ada na uboreshaji wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari.
Mragili pia alisisitiza umuhimu wa usimamizi makini wa miradi ya maendeleo, akibainisha kuwa licha ya Serikali kupeleka fedha nyingi, baadhi ya miradi imeonekana kuwa na mapungufu hasa katika hatua za umaliziaji. Alionya kuwa halmashauri haitaongeza fedha nje ya bajeti iliyopangwa, hivyo miradi inapaswa kukamilika kwa ubora unaostahili kulingana na fedha zilizotengwa.
Katika kuongeza mapato ya ndani, Mkuu huyo wa Wilaya alipendekeza kutengwa kwa eneo maalum la maegesho ya malori yanayotoka Dar es Salaam kuelekea nchi jirani za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na Burundi. Alisema kwa sasa malori hayo hulazimika kuegesha kando ya barabara kuu katika maeneo ya Ushirombo na Uyovu, jambo ambalo linaweza kugeuzwa kuwa fursa ya mapato iwapo eneo rasmi la maegesho litatengwa na kusimamiwa vizuri.
Utekelezaji wa mradi wa Zahanati ya Igulwa unatarajiwa kuleta nafuu kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo jirani kwa kupata huduma za afya karibu zaidi.

Comments
Post a Comment