Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita imejiwekea lengo la kukusanya mapato ya ndani kiasi cha shilingi bilioni 4.9 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo ilipanga kukusanya shilingi bilioni 4.3.
Hayo yameelezwa na Afisa Mipango wa Wilaya ya Bukombe, Kikonge Jeremiah, wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027. Baraza hilo limeipitisha bajeti hiyo kwa kauli moja, likionesha dhamira ya kuendelea kusukuma mbele maendeleo ya wananchi.
Jeremiah alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027, halmashauri imepitisha bajeti ya jumla ya shilingi 52,865,618,894.64, ikijumuisha mishahara ya watumishi. Kati ya fedha hizo, mapato ya ndani shilingi 4,985,027,894.64.
Alibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, halmashauri ilipitisha bajeti ya jumla ya shilingi bilioni 50,761,212,999.99, huku mapato ya ndani yakiwa shilingi bilioni 4,364,866,000.00. Ongezeko hilo la mapato ya ndani linatarajiwa kuchochea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.
Wakati wa mjadala wa bajeti kabla ya kuipitisha, Diwani wa Viti Maalum, Pili Kondela, alishauri halmashauri ielekeze sehemu ya mapato ya ndani katika ujenzi wa machinjio ya kisasa eneo la Mwalo badala ya kutenga fedha za ukarabati kila mwaka.
Aidha, Kondela alipendekeza pia fedha zitengwe kwa ajili ya ukarabati wa shule za msingi, akitaja Shule ya Msingi Butubili kuwa miongoni mwa shule zinazohitaji maboresho ya haraka.
Diwani wa Kata ya Ushirombo, Lameck Waragi, aliunga mkono hoja ya ujenzi wa machinjio ya kisasa Mwalo, akisema hatua hiyo itaondoa gharama kubwa zinazotumika kila mwaka kwenye ukarabati.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bulangwa, Yusuph Mohamed, aliomba halmashauri itenge shilingi milioni 500 kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa Zahanati ya Butinzya.
Akizungumza baada ya bajeti kupitishwa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukombe, Erick Kagoma, alifafanua kuwa halmashauri imeweka kipaumbele maalum kwenye ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Zahanati ya Msonga.
Kagoma alisema kuwa halmashauri imekuwa ikitekeleza kipaumbele hicho kila mwaka wa fedha, hivyo haiwezekani kuhamisha shilingi milioni 70 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa chumba hicho na kuzipeleka kwenye machinjio, ukarabati wa shule au zahanati nyingine.
Aliwaomba wataalamu wa halmashauri kushirikiana kwa karibu na madiwani katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuhakikisha halmashauri inafikia malengo iliyojiwekea.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bukombe, Merania Kwai, alilihakikishia Baraza la Madiwani kuwa wataalamu wataendelea kutekeleza bajeti kwa ushirikiano na madiwani ili kufikia malengo ya maendeleo kwa wananchi.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe, Ally Mketo, aliwapongeza madiwani kwa kupitisha bajeti yenye vipaumbele vinavyogusa maisha ya wananchi moja kwa moja kwa kuwasogezea huduma za kijamii.
Mketo aliwahimiza madiwani kuwa mabalozi wa uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, akieleza kuwa bima hiyo inanufaisha kaya kwa kutoa huduma kwa hadi watu sita wenye umri wa chini ya miaka 21, pamoja na kugharamia huduma za upasuaji hadi mara 36 kuanzia ngazi ya zahanati hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili, sambamba na upatikanaji wa vifaa tiba 247 kwa mgonjwa.
Akihitimisha kikao cha Baraza la Bajeti, Mwenyekiti wa Halmashauri, Erick Kagoma, alisema pamoja na bajeti kuu, baraza hilo pia limepitisha bajeti ya TARURA yenye jumla ya shilingi bilioni 5.3, huku Bajeti ya shilingi bilioni 1.3 zikihusishwa na utekelezaji wa miradi ya RUWASA.

Comments
Post a Comment