Na, Ernest Magashi
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita (GEREFA) kimepiga marufuku kwa kocha yeyote asiye na leseni halali ya ukocha kusimama kwenye benchi la ufundi katika mashindano yote yanayosimamiwa na GEREFA na GEDFA, kwa kuzingatia sheria na kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa GEREFA, Salum Kulunge, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa makocha 57 waliohitimu mafunzo ya ukocha ngazi ya Grassroots yaliyofanyika mkoani Geita.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kulunge alisema ni wajibu wa kila timu na kituo cha kulea vipaji kuhakikisha wanakuwa na makocha wenye leseni halali ili kuimarisha taaluma ya ukocha na kukuza vipaji vya wachezaji kwa kuzingatia misingi na viwango vinavyotambuliwa kisheria.
Aidha, aliwataka makocha waliopata vyeti kutumia ipasavyo elimu waliyoipata kwa kuendeleza nidhamu, weledi na uadilifu katika kazi yao, huku akizitaka timu zote zinazoshiriki mashindano chini ya GEREFA na GEDFA kutekeleza agizo hilo mara moja.
GEREFA imeeleza kuwa haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya timu au makocha watakaokiuka maelekezo hayo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha maendeleo ya soka mkoani Geita na kuhakikisha kanuni za TFF zinafuatwa kikamilifu.

Comments
Post a Comment