Wananchi wametakiwa kuachana kabisa na vitendo vya unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na ugonjwa wa kifafa, na badala yake kuwajali, kuwapa heshima na msaada unaostahili kama sehemu ya jamii.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kifafa Duniani yaliyofanyika Februari 06, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Dkt. Samizi alisema kuwa unyanyapaa umekuwa chanzo kikubwa cha wagonjwa wa kifafa kushindwa kupata ushirikiano kutoka kwa familia na jamii zinazowazunguka, hali inayosababisha wengi kuchelewa kupata matibabu na kufika hospitalini wakiwa katika hali mbaya kiafya.
Aliongeza kuwa Wizara ya Afya inaendelea kuandaa na kutekeleza miongozo na taratibu mbalimbali zitakazohakikisha wagonjwa wa kifafa nchini wanaishi katika mazingira salama, yenye staha na bila kunyanyapaliwa.
“Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa watu takribani milioni 50 duniani wanaishi na kifafa, huku watu milioni 6 wakigundulika kila mwaka. Watu wenye kifafa wako katika hatari ya vifo mara tatu zaidi ikilinganishwa na watu wengine, huku Afrika ikiripoti viwango vya vifo mara nne hadi sita. Zaidi ya asilimia 80 ya mzigo wa kifafa duniani unabebwa na nchi zenye kipato cha chini na cha kati, ikiwemo Tanzania,” alisema Dkt. Samizi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Julieth Magandi, alisema kuwa unyanyapaa bado ni changamoto kubwa kwa wagonjwa wa kifafa kutokana na imani potofu zilizojengeka katika baadhi ya jamii kuwa kifafa ni kurogwa, laana au ugonjwa wa kurithi, jambo ambalo si la kweli kitaalamu.
Dkt. Magandi alisisitiza kuwa kifafa ni ugonjwa unaotibika na kudhibitika kwa matibabu sahihi, hivyo jamii inapaswa kuachana na mila na dhana potofu na badala yake kuwapatia wagonjwa wa kifafa msaada, ulinzi na heshima wanayostahili.
Aidha, akiwasilisha mada katika maadhimisho hayo, Rais wa Chama cha Kifafa nchini, Profesa William Matuja, alisema elimu kwa jamii ni nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya kifafa, akibainisha kuwa jamii ikielimishwa ipasavyo, wagonjwa wengi watajitokeza mapema kupata matibabu na kuishi maisha ya kawaida kama wananchi wengine.

Comments
Post a Comment