DKT. BITEKO AWAPONGEZA WATAALAMU NA WALIMU KWA MATOKEO BORA YA KIDATO CHA NNE


Na, Ernest Magashi

Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Doto Biteko, amewapongeza wataalamu na walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita kwa ushirikiano wao mzuri uliowezesha wilaya hiyo kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2025.Dkt. Biteko alitoa pongezi hizo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na mshikamano kati ya wataalamu wa idara mbalimbali, walimu wa shule za msingi na sekondari, pamoja na viongozi wa ngazi ya vijiji na kata.“Nawapongeza sana wataalamu wa idara zote. Walimu wamekuwa wakijituma kutimiza wajibu wao mashuleni na matokeo mazuri tunayoyaona ni ushahidi wa kazi kubwa inayofanywa. Waheshimiwa madiwani, endeleeni kushirikiana na wataalamu, kwani mafanikio yote ya maendeleo yanayotokea Bukombe yanatokana na juhudi zao,” alisema Dkt. Biteko.Aliwahimiza madiwani na wataalamu kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan katika sekta ya elimu. Aidha, aliwataka kuhamasisha wazazi na walezi kuwekeza katika elimu kwa kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shule kwa wakati.Dkt. Biteko alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu na kuweka mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia, hivyo jamii inapaswa kuunga mkono juhudi hizo.Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, akizungumza kwa niaba ya wataalamu, alisema wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kushirikiana na madiwani ili kufikia malengo ya Serikali katika sekta ya elimu na maendeleo kwa ujumla.Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, Erick Kagoma, aliwasisitiza madiwani kuongeza juhudi katika mikutano ya hadhara ili kuhamasisha wazazi na walezi kupeleka watoto shule kabla ya kuanza kwa msako uliotangazwa na Mkuu wa Wilaya.Awali, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadis Paskas Mragili, aliwataka madiwani kuhamasisha wazazi kupeleka watoto waliofikia umri wa kuanza darasa la awali na la kwanza, pamoja na wanafunzi wa kidato cha kwanza kuripoti shule kwa wakati.Alisisitiza pia umuhimu wa kudhibiti utoro shuleni kwa kushirikiana na wazazi na walezi, akieleza kuwa ni wajibu wa mzazi au mlezi kuhakikisha mtoto anafuatiliwa maendeleo yake kabla ya kufikia siku 90 za kisheria za kufutwa jina shuleni kutokana na kutohudhuria masomo.

Comments