Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Naibu Waziri Mkuu msitafu Dkt. Doto Biteko, amewapongeza madiwani pamoja na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe kwa ushirikiano mzuri wanaouonyesha katika kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali.
Pongezi hizo amezitoa katika kikao cha Baraza la Madiwani, wakati madiwani wakisoma taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kata zote 17 za wilaya hiyo. Taarifa hizo zimeonesha kuwepo kwa ushirikiano mzuri kati ya madiwani, wataalamu na wananchi, huku wananchi wakishiriki kwa kuchangia nguvu zao katika utekelezaji wa miradi.
Dkt. Biteko aliwashukuru madiwani kwa kuendelea kuhamasisha wananchi kujitolea kushiriki katika miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana kwa jitihada za Serikali pekee bila ushiriki wa wananchi.
“Niwapongeze sana madiwani na wataalamu wa Halmashauri ya Bukombe kwa ushirikiano mkubwa mnaouonesha katika kusimamia miradi ya maendeleo inayopata fedha nyingi kutoka Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Naona miradi inaendelea vizuri; endeleeni kuwaza mbele zaidi kwa ajili ya kuijenga Bukombe,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo umechangia utekelezaji wa miradi kwa ufanisi na ubora, hali inayosababisha kuwepo kwa fedha zinazobaki kwenye baadhi ya miradi na hivyo kuongeza hamasa kwa wananchi kuendelea kujitoa.
Awali, Diwani wa Kata ya Ng’anzo, Mashaka Shig’wenda, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya kata hiyo, aliipongeza Serikali kwa kuleta fedha za miradi ya maendeleo hususani katika sekta za elimu na afya.
Shig’wenda amesema pamoja na Serikali kuleta fedha, Mbunge Dkt. Biteko amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na wananchi kwa kuchangia mabati na matofali katika miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, aliwashukuru madiwani kwa taarifa zao na kuahidi kuwa wataalamu wataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, akizungumza kwa niaba ya madiwani, amesema watahakikisha wanaendelea kushirikiana kwa karibu na wataalamu kama walivyosisitizwa, ili kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Comments
Post a Comment