DKT. BITEKO ASHUHUDIA UTIAJI SAINI UBIA MKUBWA WA UCHIMBAJI DHAHABU KATI YA STAMICO NA PLANTCOR YA AFRIKA KUSINI
Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dkt. Doto Biteko, ameshuhudia hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ubia wa uchimbaji wa madini ya dhahabu kati ya Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) na kampuni ya PLANTCOR ya Afrika Kusini.
Ubia huo unahusisha utafiti na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika leseni saba zinazomilikiwa na STAMICO zilizopo eneo la Kigos, wilayani Bukombe. Hafla hiyo imefanyika Februari 24, 2026, katika wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Biteko aliwataka wananchi wa Bukombe kuendelea kubuni na kutumia fursa za kiuchumi zitakazotokana na uwekezaji huo mkubwa, akisisitiza kuwa wilaya hiyo inaelekea kufunguka zaidi kiuchumi. Pia alisisitiza umuhimu wa wawekezaji kuwa na mahusiano mazuri na wananchi ili kuhakikisha maendeleo yanakuwa shirikishi.
Aidha, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini, hali inayochangia Bukombe kuwa sehemu ya uchumi mkubwa wa madini. Alilipongeza Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) kwa kufanikisha hatua hiyo muhimu ya kimkakati.
Dkt. Biteko pia aliwapongeza wawekezaji wa PLANTCOR kwa kueleza kuwa mbali na kufanya utafiti katika leseni za STAMICO, wako tayari kushirikiana na wachimbaji wengine kwa kuwapatia taarifa sahihi za kitaalamu ili kuepusha uchimbaji wa kubahatisha katika eneo la Kigos.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, alisema shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji na kusimamia utekelezaji wa mkataba kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla. Alitoa shukrani kwa viongozi na wadau wote waliohudhuria hafla hiyo na kumshukuru Mungu kwa kufanikisha tukio hilo muhimu.
Kwa upande wake, Katibu wa kampuni ya uchimbaji madini PLANTCOR Mhadis Joseph Wilimas, aliishukuru Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiamini kampuni hiyo na kuipa fursa ya kuwekeza nchini. Aliahidi kuwa kampuni hiyo itazingatia sheria, kanuni na taratibu zote za nchi, ikiwemo utunzaji wa mazingira na kuendeleza mahusiano mazuri na Serikali pamoja na wananchi wanaozunguka eneo la mradi.
Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Simon Siro, alisema tukio hilo ni la kihistoria na litaongeza thamani ya sekta ya madini huku likichochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi wa Bukombe. Alibainisha kuwa jitihada za Serikali katika kudhibiti vitendo vya uhalifu zimewezesha mazingira kuwa salama na rafiki kwa uwekezaji.
Naye Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Stivin Kiruswa, alisema PLANTCOR ni miongoni mwa kampuni kubwa barani Afrika zinazotoa huduma za uchimbaji wa madini ya dhahabu. Alieleza kuwa kupitia makubaliano hayo, leseni saba za STAMICO zitafanyiwa utafiti wa kina ili kufikia lengo la kuanzisha mgodi mkubwa wa dhahabu kupitia ubia huo.
Dkt. Kiruswa aliongeza kuwa mgodi huo utakapoanza uzalishaji utatoa ajira kwa wananchi wa Bukombe, kuongeza mzunguko wa fedha katika jamii na kuchochea utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR). Pia aliitaka kampuni ya PLANTCOR kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapatiwa njia za kupita kuelekea maeneo yao ya leseni, huku Wizara ikiendelea kulinda maslahi mapana ya taifa.
Alihitimisha kwa kuwataka wawekezaji kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba, huku STAMICO ikiendelea kushirikiana nao kwa karibu ili kuhakikisha mradi unaleta tija kwa taifa na wananchi wa Bukombe.

Comments
Post a Comment