Diwani wa Kata ya Bugelenga mkoani Geita, Donald Lubigisa, kwa kushirikiana na wananchi wa kata hiyo, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Doto Biteko, kwa juhudi zake za kufuatilia na kuleta fedha za miradi ya maendeleo katika eneo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Lubigisa amesema Dkt. Biteko amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Serikali inaleta shilingi milioni 351 kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa barabara inayounganisha Wilaya ya Bukombe na Wilaya ya Mbogwe, kuanzia Msasani hadi Mkange.
Amesema hatua hiyo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Mbunge huyo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kupeleka fedha za maendeleo ili kuboresha miundombinu na kuinua maisha ya wananchi.
Mkazi wa Bugelenga, Thomas Shigata, amesema hapo awali wananchi walikumbana na changamoto kubwa ya kusafirisha mazao yao hasa kipindi cha mvua za masika, kutokana na mto na maeneo ya mabondeni kujaa maji. Hali hiyo ilisababisha kushuka kwa uzalishaji na kuongeza gharama za usafiri, huku baadhi yao wakilazimika kuzungukia Ushirombo kwenda Masumbwe kwa gharama kubwa zaidi.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Msoka Msumba, amesema mradi huo wa shilingi milioni 351 umeletewa na Serikali kwa lengo la kuboresha miundombinu na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao.
Ameeleza kuwa ukarabati huo unahusisha kunyanyua matuta katika maeneo matatu korofi, uwekaji wa changarawe kwa umbali wa kilomita 10 pamoja na uwekaji wa makalvati tisa. Ameongeza kuwa mradi unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika ndani ya muda uliopangwa.
Mhandisi Msumba amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea shughuli za kiuchumi, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuinua kipato cha wananchi wa Bugelenga na maeneo jirani.

Comments
Post a Comment