DC AWATAKA MADIWANI KUHAMASISHA WAZAZI KUPELEKA WATOTO SHULENI KABLA YA KUANZA MUSAKO


Na, Ernest Magashi

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wametakiwa kuhamasisha wazazi na walezi kuhakikisha watoto waliofikia umri wa kuanza shule wanaripoti kwa wakati, kabla ya kuanza kwa msako wa kuwachukulia hatua wazazi watakaokaidi agizo hilo.Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadis Paskas Mragili, wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani. Amesema amepokea taarifa kuwa kasi ya uandikishaji na uripoti wa wanafunzi, hususan wa darasa la awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza, bado hairidhishi.Ameeleza kuwa idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza walioripoti shuleni iko chini ya asilimia 80 ukilinganisha na idadi ya waliofaulu darasa la saba mwaka jana.“Waheshimiwa madiwani, nawaombeni sana muhamasishe wazazi na walezi wapeleke watoto shule. Tumeanza mwaka vizuri tangu shule zilipofunguliwa Januari 2026, lakini mwitikio wa darasa la awali, la kwanza na kidato cha kwanza bado ni mdogo. Kuanzia wiki ijayo, kila mzazi au mlezi mwenye mtoto aliyeandikishwa na hajafika shule atachukuliwa hatua kupitia serikali za vijiji na kata,” alisisitiza Mragili.Aliongeza kuwa Serikali imeboresha miundombinu ya kujifunzia na inaendelea kutekeleza Sera ya Elimu Bila Malipo, hivyo jukumu la mzazi ni kuhakikisha mtoto anapata haki yake ya elimu. Alionya kuwa Serikali haitavumilia kuona watoto wanabaki nyumbani bila sababu za msingi, na wazazi watakaobainika watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.Mkuu huyo wa wilaya alisema licha ya Bukombe kufanya vizuri kitaaluma mkoani Geita, juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shuleni ili kufikia lengo la Serikali la kutoa elimu bora kwa kila mtoto.Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Naibu Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Doto Biteko, aliwapongeza wataalamu wa idara mbalimbali, hususan za elimu ya msingi na sekondari, kwa juhudi zao zilizoifanya wilaya hiyo kushika nafasi ya kwanza kimkoa katika matokeo ya mitihani.Dkt. Biteko aliwahimiza madiwani na wataalamu kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhamasisha wazazi kusomesha watoto wao ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwemo sekta ya elimu.Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, aliahidi kuwa wataalamu wataendelea kushirikiana na madiwani kuhakikisha malengo ya elimu yanafikiwa.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri, Erick Kagoma, aliwataka madiwani kwenda kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao kuhamasisha wazazi na walezi kupeleka watoto shule kabla ya kuanza rasmi kwa msako huo.

Comments