Watumishi wa umma wilayani Bukombe, mkoani Geita, kuanzia ngazi ya kijiji hadi Wilaya, wametakiwa kutenga muda kwa ajili ya mazoezi ya viungo ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe (DAS), Ally Mketo, wakati wa bonanza la watumishi wa umma lililofanyika katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Ushirombo. Mketo alisema mazoezi ni sehemu muhimu ya kujenga afya bora na kuongeza ufanisi kazini.
Alisisitiza kuwa mazoezi ya mara kwa mara husaidia kujikinga na kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo, ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.
“Afya njema ni mtaji wa kazi bora. Kupitia mazoezi ya mara kwa mara tunaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa hatari ya magonjwa yasiyoambukiza,” alisema Mketo.
Aidha, alieleza kuwa bonanza hilo limeandaliwa kwa lengo la kuimarisha mshikamano miongoni mwa watumishi wa idara mbalimbali, pamoja na kuhamasisha mtindo bora wa maisha.
Kwa upande wake, Afisa Michezo wa Wilaya ya Bukombe, Jenipha Kisusi, aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kwa ushirikiano walioutoa katika maandalizi ya bonanza hilo.Alisema tukio hilo limewapa watumishi fursa ya kushiriki michezo, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kazini.
Kisusi alibainisha kuwa bonanza lilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kuvuta kamba, mbio fupi na mchezo wa kukimbiza kuku, ambapo washiriki walionesha ushindani mkubwa wahali ya juu.
Katika mchezo wa mpira wa miguu, watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe waliibuka washindi kwa kuichapa timu ya Serikali Kuu mabao5-0.
Mmoja wa washiriki wa mchezo wa kukimbiza kuku alisema mchezo huo unapaswa kuandaliwa mara kwa mara kwani mbali na burudani, hutoa motisha kwa washiriki kupitia zawadi mbalimbali ikiwemo vifaa vya michezo na bahasha za fedha.

Comments
Post a Comment