WAZAZI NA WALEZI WAHIMIZWA KUWAANDIKISHA WATOTO SHULENI


Na, Ernest Magashi

Wazazi na walezi Wilayani Bukombe, mkoani Geita, wametakiwa kuhakikisha wanawaandikisha na kuwapeleka shule watoto wote waliofikia umri wa kuanza masomo kuanzia elimu ya awali (chekechea) hadi kidato cha kwanza.Wito huo umetolewa na Askofu wa Kanisa la Ufunuo Jimbo la Geita, Askofu Rosemary Mashauri Bendera, Jumapili ya Januari 18, 2026, wakati wa ibada ya shukrani kwa Mungu ya kuvuka mwaka 2025 na kuingia mwaka 2026, iliyofanyika katika Kanisa la Ufunuo mjini Ushirombo, wilayani Bukombe. Katika ibada hiyo, Askofu Rosemary aliipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo.Askofu Rosemary aliwahimiza waumini wa Jimbo la Geita kuwekeza katika elimu ya watoto wao, akisisitiza kuwa Serikali imeendelea kujenga shule mpya na kukarabati miundombinu ya elimu ili wanafunzi wasome katika mazingira rafiki kupitia mpango wa elimu bila malipo.“Nawasihi wapendwa, tusipuuzie elimu. Hakikisheni mnasomesha watoto wenu. Serikali kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, inaendelea kupambana kutafuta fursa za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Askofu Rosemary.Aidha, alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo, huku akiwahimiza wananchi kushirikiana kwa pamoja katika kuijenga na kuendeleza wilaya ya Bukombe.Askofu Rosemary pia aliwaomba waumini kuendelea kuiombea Serikali na viongozi wake ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, akitaja miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa wilayani Bukombe ikiwemo ujenzi wa soko la kisasa, stendi ya mabasi na uwanja wa mpira wa miguu.Katika ibada hiyo, Askofu Rosemary aliwatunuku wachungaji 12 daraja la uchungaji kamili na kuwakabidhi vifaa vya kazi ili waweze kumtumikia Mungu kwa kushirikiana na Serikali pamoja na jamii zinazowazunguka katika vituo watakavyopangiwa.Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu Rosemary aliwashukuru wachungaji wasaidizi na viongozi mbalimbali kwa kushiriki ibada ya kuanza mwaka mpya, akimshukuru pia Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufunuo Tanzania, Dkt. Paul Bendera, kwa kumuamini na kumpa jukumu la utumishi. Aidha, aliwasisitiza waumini, wachungaji na makundi yote ndani ya Kanisa kuendeleza upendo, mshikamano na umoja katika kutimiza kazi ya Mungu kwa kuzingatia misingi ya kanisa.Akizungumza kwa niaba ya wachungaji waliotawazwa, Mchungaji Samwel Cosmas alisema watazingatia na kuyaishi mafundisho pamoja na kiapo cha maadili kwa kufuata mwongozo na katiba ya Kanisa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, katika ziara zake za kikazi hivi karibuni amekuwa akihamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo kwa kuchangia nguvu kazi katika ujenzi wa zahanati na shule.Dkt. Biteko alisema Serikali inatarajia kukarabati shule 23 pamoja na miundombinu yake, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za elimu, huku jukumu la wazazi na walezi likibaki kuwa ni kuhakikisha watoto wote wanapelekwa shule.Ibada hiyo ilihudhuriwa pia na Mchungaji Mwangarizi Nguzo Bendera ,  Mchungaji  Mwangarizi  Grece Bendera pamoja na viongozi wengine waalikwa.

Comments