Watoa huduma za chanjo katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya wilayani Bukombe mkoani Geita wamehimizwa kutoa huduma kwa ufanisi na kwa kuzingatia mafunzo waliyopewa, ili kuboresha utoaji wa chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili kuhusu matumizi ya Mfumo Jumuishi wa Kielektroniki wa Usajili wa Watoto na Utoaji Chanjo (iTImR). Mafunzo hayo yalilenga kuboresha ubora wa ukusanyaji na uhifadhi wa takwimu za chanjo katika ngazi ya vituo vya afya.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mfikwa aliwataka watoa huduma kutumia mfumo huo ipasavyo kama walivyoelekezwa, ili kuhakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi na za kuaminika.
“Ni muhimu kutumia mfumo huu kama mlivyoelekezwa ili kuhifadhi taarifa kwa usahihi na kupata takwimu sahihi za chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano,” alisema Mfikwa.
Aidha, aliwahimiza watoa huduma kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na kwa mapenzi makubwa ili kutimiza malengo ya Serikali katika sekta ya afya. Alisisitiza kuwa endapo kutajitokeza changamoto yoyote wakati wa matumizi ya mfumo huo, wahusika wasisite kutoa taarifa kwa Maafisa TEHAMA kwa ajili ya ufumbuzi wa haraka.
Vilevile, Mfikwa aliwataka wahudumu hao kuhakikisha wanavitunza vishikwambi walivyokabidhiwa ili vidumu kwa muda mrefu, akitumia msemo usemao “Kitunze kikutunze.”
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Dkt. Deograsia Mkapa, aliishukuru Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa kushirikiana na TAMISEMI kwa kufanikisha mafunzo hayo pamoja na kutoa vishikwambi 36 vitakavyotumika kama vifaa muhimu vya ukusanyaji wa takwimu na utoaji wa taarifa za chanjo

Comments
Post a Comment