Wananchi wa kijiji cha Buganzu, kata ya Uyovu wilayani Bukombe mkoani Geita, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuanza kutekeleza ahadi zake kupitia ukarabati wa Shule ya Msingi Buganzu.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Buganzu, Peter Nkinga, pamoja na Diwani wa Kata ya Uyovu, Mathayo Kagoma, wakati wa ziara ya kutembelea shule hiyo ambayo imepokea shilingi milioni 101 kutoka Serikalini kwa ajili ya ukarabati.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti Peter alisema kuwa mbunge kwa kushirikiana na Serikali amehakikisha wananchi wanapata huduma bora, ikiwemo sekta ya elimu, huku shule hiyo ikinufaika na fedha za ukarabati kama sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Dkt. Biteko.
“Wananchi wa kijiji hiki wanatambua mchango mkubwa wa Serikali na Mbunge wetu katika kuboresha huduma za elimu,” alisema Peter.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Buganzu, James Jororo, alisema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 2,137 na kutumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuanzisha shule nyingine kijijini hapo ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Aliongeza kuwa ukarabati unaoendelea umeboresha kwa kiasi kikubwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia, ikilinganishwa na hali ya awali ya uchakavu.
Diwani wa Kata ya Uyovu, Mathayo Kagoma, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bukombe kuleta fedha shilingi milioni 101 kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Msingi Buganzu.
Akielezea historia ya shule hiyo, Mathayo alisema ujenzi wake ulianza kwa nguvu za wananchi, ambapo Mbunge Dkt. Doto Biteko aliunga mkono juhudi hizo kwa kutoa mabati pamoja na mifuko 100 ya saruji, hali iliyopelekea shule kusajiliwa rasmi na kuanza kupokea wanafunzi.
Aidha, alisema Serikali kupitia Mradi wa BOOST imeleta fedha kwa ajili ya ukarabati wa vyumba tisa vya madarasa na ofisi moja ya walimu, huku mradi huo ukiwa katika hatua za mwisho na ukijumuisha uwekaji wa nishati ya umeme shuleni hapo.
Mathayo Kagoma alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Diwani, Mbunge na Serikali umeendelea kuleta maendeleo kwa wananchi, na kuwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili miradi mingine ya maendeleo iendelee kutekelezwa.

Comments
Post a Comment