Wananchi wa Kijiji cha Ilyamchele, Kata ya Namonge wilayani Bukombe mkoani Geita, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha za maendeleo kiasi cha shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho.
Pongezi hizo zimetolewa na mkazi wa kijiji hicho, Neema Charles, wakati wa ziara ya Diwani wa Kata ya Namonge aliyekagua mradi huo wa ujenzi, kufuatia Serikali kutoa fedha hizo ili kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Charles alimpongeza Mbunge Dkt. Biteko kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo, akisema tunamatimaini makibwa na mbunge kwenye kuleta maendeleo kwa vitendo, hususani katika sekta ya afya.
Akizungumza katika ziara hiyo, Diwani wa Kata ya Namonge, Mlalu Bundala, amesema awali kata hiyo haikuwa na Kituo cha Afya, lakini kupitia ushirikiano wa Mbunge Dkt. Biteko na wananchi, Kituo cha Afya kilijengwa na sasa wananchi wanapata huduma bora zaidi. Ameongeza kuwa juhudi hizo zimeendelea kwa ujenzi wa zahanati mbalimbali ikiwemo Zahanati ya Ilyamchele.
“Namshukuru Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa jitihada zake kubwa za kuimarisha huduma za afya kwa wananchi. Ushirikiano wake na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umeleta utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo katika kata yetu, ikiwemo kupatikana kwa fedha za kukamilisha Zahanati ya Ilyamchele,” amesema Bundala.
Ameeleza kuwa mradi huo ulianza kwa nguvu za wananchi, ambapo Mbunge Dkt. Biteko aliunga mkono jitihada hizo kwa kuchangia mabati 220 pamoja na shilingi milioni 14, hatua iliyochochea kasi ya ujenzi na ushiriki mkubwa wa wananchi.
Bundala ameongeza kuwa wakati wa ziara ya Mbunge katika Kata ya Namonge mwezi Julai 2024, alikuta wananchi wa Kijiji cha Ilyamchele wakiwa tayari wameanza ujenzi wa zahanati kwa michango yao wenyewe, ndipo alipotoa msaada huo wa fedha na mabati uliosaidia kukamilisha hatua muhimu za ujenzi.
Baada ya hatua hizo, amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa shilingi milioni 60 kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo ili huduma za afya zianze kutolewa kwa wananchi wa kijiji hicho, ambao kwa muda mrefu walilazimika kutembea umbali wa takribani kilomita 20 kwenda na kurudi kufuata huduma katika Kituo cha Afya Namonge.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Ujenzi wa Zahanati hiyo, Dkt. Ezekia Mollel, amesema fedha hizo tayari zimeingizwa kwenye akaunti ya mradi na vifaa vyote muhimu vimeshanunuliwa. Ameongeza kuwa fundi anaendelea na kazi na kuahidi kuwa ujenzi utakamilika kwa haraka ili huduma za afya zianze kutolewa kwa wananchi.

Comments
Post a Comment