Wananchi wa kijiji cha Itunga, kata ya Bukombe wilayani Bukombe mkoani Geita, wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa kuwapatia vifaa vya ujenzi vikiwemo bati, mbao, misumari na saruji kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho.
Pongezi na shukrani hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na wananchi mara baada ya Mbunge huyo kukabidhi vifaa hivyo vya ujenzi, hatua iliyorejesha matumaini ya kukamilika kwa mradi uliokuwa umekwama kwa muda mrefu.
Mkazi wa kijiji hicho, Sabina Mhoja, akitoa shukrani zake alisema Dkt. Biteko ameonyesha imani kubwa kwa wananchi na kugusa moja kwa moja mahitaji yao, hususan katika sekta ya afya, kwani kukamilika kwa Zahanati hiyo kutaondoa adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Sabina aliongeza kuwa ujenzi wa Zahanati hiyo ulianzishwa kwa nguvu za wananchi lakini ulikwama kutokana na ukosefu wa vifaa, hali iliyobadilika baada ya Mbunge huyo kutoa msaada wa ukamilishaji.
“Ninamshukuru sana Mbunge Dkt. Doto Biteko kwa kutuletea vifaa vya kukamilisha ujenzi wa Zahanati. Mradi huu ukikamilika utasaidia wananchi kuacha kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya,” alisema Sabina.
Naye Paulina Masalu alimpongeza Mbunge huyo kwa kuonyesha ushirikiano wa dhati na wananchi kwa kuwaletea vifaa vya ujenzi ambavyo hawakuwa na matarajio ya kuvipata kwa wakati huu. Alisema Dkt. Biteko amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wananchi kuibua na kushiriki katika miradi ya maendeleo, na amekuwa mfano bora wa uongozi unaowajali wananchi.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Itunga, Emmanuel Kamoli, alisema ujenzi wa Zahanati hiyo ulikuwa umekwama kwa zaidi ya miaka minane, lakini ujio wa Mbunge umeufufua na kuupa uhai mpya.
“Tumepokea bati 250, mbao,580 mifuko 200 ya saruji, misumari pamoja na fedha Sh 1.3 milioni kwa ajili ya fundi. Kwa kushirikiana na wajumbe wa serikali ya kijiji, tutasimamia vyema ujenzi ili wananchi waanze kupata huduma za afya karibu,” alisema Kamoli.
Kamoli aliongeza kuwa kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Itunga, wanamshukuru Dkt. Biteko kwa kuwa mkombozi wa afya zao, kwani Zahanati hiyo sasa inaelekea kukamilika kwa kipindi kifupi kutokana na msaada huo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, alisema ametoa msaada huo kama sehemu ya kutekeleza ahadi zake kwa wananchi na akaahidi kuendelea kuwaunga mkono katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Biteko pia aliwahimiza wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema Rais anawapenda wananchi na ndiyo maana anaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Comments
Post a Comment