WANANCHI WAHIMIZWA KUJITOLEA NGUVU ZAO KWENYE MIRADI YA MAENDELEO


Na, Ernest Magashi

Wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamehimizwa kuendelea kudumisha umoja na mshikamano kwa kujitolea nguvu zao katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususani kwa kuchangia nguvu kazi kama kusogeza mchanga, mawe na zege wakati wa ujenzi wa miradi ya afya.Wito huo umetolewa l na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, leo Januari 6,2026 alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Itunga, Kata ya Bukombe, mara baada ya kukabidhi bati 250, mbao 580 pamoja na misumari kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho.Dkt. Biteko alisema ni muhimu kwa wananchi wa Bukombe kushikamana na kuendelea kujitoa katika miradi ya maendeleo ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuleta tija kwa jamii. Alisisitiza kuwa jitihada za wananchi zitasaidia Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuendelea kuleta fedha za maendeleo wilayani humo.“Mradi huu wa zahanati ulianza mwaka 2018 na hadi sasa bado haujakamilika. Imepita miaka takribani nane, hali ambayo siyo nzuri. Nimekuja leo kukabidhi vifaa hivi kama sehemu ya kutimiza ahadi niliyotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Rais Samia anatupenda wananchi wa Bukombe na ndiyo maana ametupatia fedha za miradi ya maendeleo,” alisema Dkt. Biteko.Aliongeza kuwa hatamani kuona ujenzi wa zahanati hiyo unasimama tena, bali ukamilike ili wananchi wa kijiji cha Itunga na maeneo ya jirani waweze kupata huduma za afya karibu na makazi yao.Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bukombe, Rozaria Masokola alimshukuru Mbunge kwa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo na kwa wakati, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kumuunga mkono Mbunge wao kwa kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo.Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Itunga, Emmanuel Kamoli, alimpongeza Dkt. Biteko kwa kuwaletea vifaa vya ujenzi, akisema vitasaidia kukamilisha mradi huo kwa haraka.

Kamoli alisema kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya kutokana na kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo, lakini kwa msaada huo wanatarajia kuondokana na adha hiyo.

Comments