WANANCHI WAENDELEA KUMPONGEZA DKT. BITEKO KWA KUUNGA MKONO UJENZI WA ZAHANATI


Na, Ernest Magashi

Wananchi wa Kata ya Butinzya, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameendelea kutoa pongezi na shukrani kwa Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa mchango wake mkubwa wa kuwaunga mkono katika ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho.

Shukrani hizo zimetolewa nyakati tofauti na wananchi wa kata hiyo, kufuatia ziara ya Mbunge huyo aliyofika kushiriki moja kwa moja katika shughuli za ujenzi pamoja na kuchangia vifaa mbalimbali vya ujenzi, hatua iliyosaidia kuufufua mradi uliokuwa umekwama kwa muda mrefu.Mwananchi wa kata hiyo, Salome Mashaka, alisema hatua ya Mbunge kuwaletea vifaa vya ujenzi ni ya kupongezwa kwani itawezesha mradi huo kukamilika na kuondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Butinzya.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Butinzya, Kwizi Chenya, akizungumza kwa niaba ya wananchi, alimpongeza Dkt. Biteko kwa mpango wake madhubuti wa maendeleo unaolenga kuinua kata hiyo pamoja na Wilaya ya Bukombe kwa ujumla. Alisema ushirikiano wa Mbunge na wananchi umeleta matumaini mapya katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.Kwizi aliwahimiza wananchi kuendelea kumuunga mkono Mbunge kwa kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo, ili kuwezesha kupatikana kwa fedha za kukamilisha miradi iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi.Akizungumza wakati wa kushiriki ujenzi huo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kuonesha mshikamano katika utekelezaji wa mradi huo wa kijamii.

Aidha, aliwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa ndiye anayeendelea kutenga na kuleta fedha za maendeleo zinazotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Comments