Wachimbaji wadogo wanaofanya shughuli zao katika mgodi wa Msasa uliopo Kata ya Runzewe Magharibi, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wametakiwa kuwa watulivu, wasikivu na kufuata maelekezo ya Serikali kwa kuzingatia usalama wao, hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadis Paskas Mragili, kupitia mawasiliano ya simu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kufuatia tukio la wachimbaji kutawanywa na vyombo vya ulinzi na usalama, huku kukizuka madai kuwa risasi za moto zilitumika.
Akifafanua tukio hilo, Mragili amesema mgodi wa Msasa ulianza kazi mwezi Septemba 2025 na haujawahi kushuhudia taharuki kama hiyo. Alisisitiza kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya inafuata taratibu zote zilizopo, ikiwemo kuheshimu utaratibu wa mgodi ambao unahitaji tathmini ya wataalamu wa usalama kabla ya kuruhusu shughuli za uchimbaji kuendelea.
“Nimeona taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa mabomu na risasi za moto zilitumika, lakini ninathibitisha kuwa hakuna risasi ya moto iliyotumika. Askari walitumia mabomu ya machozi tu kwa lengo la kudhibiti hali na kuimarisha usalama wa wachimbaji,” amesema Mragili.
Aidha, Mragili amesema mgodi wa Msasa upo karibu na maeneo ya hifadhi, na usiku wa kuamkia Januari 21, 2026, mvua kubwa ilinyesha hali iliyosababisha hatari ya kujaa maji kwenye mashimo ya uchimbaji. Kutokana na hali hiyo, mmiliki wa mgodi alitoa tangazo la kusitisha shughuli za uchimbaji kwa muda kwa ajili ya usalama wa wachimbaji.
Aliongeza kuwa madai ya migogoro ya asilimia kati ya wachimbaji na mmiliki wa mgodi yanahusiana na mikataba ya awali na hayakuwa chanzo cha kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji, bali ni tahadhari ya kiusalama kutokana na mvua zinazoendelea.
“Leo hakuruhusiwa mtu yeyote kuingia mgodini, awe na mkataba au asiwe nao, kutokana na hali halisi ya maji yaliyosababishwa na mvua. Baadhi ya watu walijaribu kuvamia eneo la mgodi wakidaiwa kuiba mifuko ya mawe yenye madini ya dhahabu, ndipo askari walipochukua hatua za kuwatawanya kwa kutumia mabomu ya machozi,” amesema.
Mradi huo haujaripoti vifo vyovyote, ingawa watu wawili walipata majeraha madogo baada ya kukatwa na mabati, huku askari mmoja akiumia mkono baada ya kudondoka, na kwa sasa anaendelea vizuri kiafya.Mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali imesitisha shughuli za uchimbaji kwa muda hadi maafisa wa usalama na wataalamu wa madini watakapofika eneo hilo kufanya tathmini ya kina ya usalama, ikizingatiwa kuwa mgodi huo unaweza kuwa na wachimbaji elfu 20 kwa wakati huu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Msasa Gold Mine, Cosmos Bingo, amewaomba wachimbaji kuwa watulivu na kuheshimu sheria na taratibu za mgodi, akisisitiza kuwa usalama wa maisha ya binadamu ni kipaumbele cha kwanza.
Bingo ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano wa kiusalama inapohitajika, hasa kutokana na idadi kubwa ya watu wanaofika eneo hilo kwa shughuli za uchimbaji na biashara mbalimbali.
Naye Mkuu wa Idara ya Usalama wa Mgodi wa Msasa, James Balele, amesema idara hiyo imejipanga kikamilifu kusimamia usalama wa mashimo ya uchimbaji, na kwamba husitisha shughuli pindi wanapoona kuna hatari, ili kuzuia ajali zinazoweza kusababisha majeraha au vifo.

Comments
Post a Comment