Wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu Wilayani Bukombe mkoani Geita wameipongeza Serikali kwa kuwapatia leseni za uchimbaji, hatua ambayo wamesema imewasaidia kujikwamua kiuchumi na kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria.
Pongezi hizo zilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Msasa Gold Mine, Cosmas Ignas Bongo, wakati akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake akiwataka wachimbaji kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji ili kuepuka changamoto ikiwemo kusimamishwa kwa shughuli zao.
Bongo alisema kuwa Msasa Gold Mine imewakusanya zaidi ya wachimbaji 10,000, jambo linalohitaji nidhamu, ushirikiano na ufuataji wa maelekezo ya uongozi ili wote wanufaike na shughuli za uchimbaji.
Aliongeza kuwa ndani ya muda mfupi tangu kuanza kwa uchimbaji, wamechangia maendeleo ya jamii kwa kukarabati Ofisi ya Tarafa pamoja na kuchimba kisima kirefu cha maji safi na salama kwa ajili ya wananchi.
Aidha, aliomba Serikali ya Kijiji cha Msasa kuendelea kushirikiana na wachimbaji hao, hasa pale wanapochangia fedha katika miradi ya maendeleo, kwa lengo la kuhakikisha jamii inanufaika na rasilimali za madini.
Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Usalama wa Msasa Gold Mine, James Balele maarufu kama Ng’hwanankamba, alisema usalama katika madawati umeimarishwa, huku akibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa uchimbaji katika eneo hilo, hakuna tukio lolote la kuhatarisha usalama wa wachimbaji.
Alisema timu ya usalama hukagua zaidi ya maduwara 200 kila siku ili kuhakikisha yanafanya kazi kwa usalama na kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuepusha ajali zisizo za lazima zinazoweza kusababishwa na uzembe.
Mfanyabiashara wa nguo katika eneo hilo, Suzana Ndasa, alisema Serikali imefanya uamuzi sahihi kutoa leseni ya uchimbaji Msasa, kwani biashara yake imekua kwa kiasi kikubwa. Alisema kwa sasa anauza kati ya shilingi 700,000 hadi shilingi 1,000,000 kwa siku, tofauti na awali ambapo mauzo yalikuwa kati ya shilingi 460,000 hadi 900,000. Aliongeza kuwa ataendelea kufanya biashara kwa kufuata taratibu za uongozi na usalama ili kuongeza kipato chake.
Naye mchimbaji Paul John alisema wachimbaji wadogo wanashukuru Serikali kwa kuendelea kuwatambua na kuwapatia maeneo rasmi ya uchimbaji, hatua iliyopunguza migogoro na usumbufu uliokuwapo hapo awali.
Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, katika ziara zake za hivi karibuni jimboni humo, aliipongeza Serikali kwa kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo, akisema kuwa kila siku mji wa Runzewe Ushirombo hupokea wageni wengi, wengi wao wakiwa wachimbaji wanaokuja kutafuta dhahabu.
Dkt. Biteko amekuwa akihamasisha wananchi wa Wilaya ya Bukombe kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizotokana na kushushwa kwa eneo la Pori la Kigosi kutoka hifadhi ya TANAPA kwenda TFS, pamoja na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Madini kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo.
Mkazi wa Kijiji cha Msasa, Tomas Elisha, aliupongeza uongozi wa Msasa Gold Mine kwa kutoa maeneo ya kazi bure, huku akimpongeza pia Mbunge Dkt. Biteko kwa ushirikiano wake na Serikali uliowezesha wachimbaji kufanya shughuli zao bila bughudha kama ilivyokuwa awali.
Wakati huo huo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika Januari 15, 2025 katika Ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni jijini Dodoma, alisema Serikali imeendelea kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogo kwa kuwatengea maeneo yenye taarifa za utafiti na kuwapatia leseni za uchimbaji mdogo.
Waziri Mavunde aliongeza kuwa Wizara ya Madini imeanzisha mkakati wa Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) unaolenga kuwawezesha wachimbaji wadogo katika mitaji, teknolojia na taarifa za kijiolojia, ambapo hadi sasa zaidi ya wachimbaji 12,000 wamenufaika.
Aidha, alisema Sera ya Madini inasisitiza uwajibikaji wa kampuni za madini kwa jamii (CSR), ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya elimu, maji, barabara, afya na kilimo katika maeneo yanayozunguka migodi.

Comments
Post a Comment