Viongozi wa Serikali za Vijiji katika Kata ya Bukombe, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, wameelekezwa kuweka mikakati ya kuongeza maeneo ya zahanati ili kuwezesha kupandishwa hadhi kuwa vituo vya afya hapo baadaye.
Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, alipotembelea eneo la ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Itunga, Kata ya Bukombe. Ingawa eneo la sasa ni kubwa, Dkt. Biteko aliwataka viongozi wa Serikali ya Kijiji hicho kuhakikisha linaongezwa zaidi kwa kuzingatia mahitaji ya baadaye.
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Biteko alisema kwa sasa Kata ya Bukombe ina zahanati tano, ambapo angalau zahanati moja inapaswa kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya ili kupunguza adha ya wananchi kukosa huduma za rufaa ambazo hazipatikani katika zahanati za kawaida.
Aliongeza kuwa ni wakati sasa kwa viongozi kushirikiana na wananchi kuchangamka na kuongeza maeneo ya miradi ya maendeleo kwa kuzingatia manufaa ya muda mrefu.
“Mimi kama Mbunge nitaendelea kupambana kutafuta fursa za maendeleo kwa ajili ya wananchi wa Bukombe, huku Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiendelea kuleta fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” alisema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko aliwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kudumisha amani, mshikamano na upendo, pamoja na kumuombea ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kitaifa.
“Viongozi wa vijiji hakikisheni mnaongeza eneo la zahanati ili liwe na sifa za kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya. Rais Dkt. Samia ameendelea kuleta fedha za maendeleo kwa sababu anawapenda wananchi wa Bukombe,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Itunga, Emmanuel Kamoli, alisema Serikali ya Kijiji imeupokea ushauri wa Mbunge na itaanza kuufanyia kazi kwa kuzungumza na wamiliki wa maeneo yanayozunguka zahanati hiyo.
Kamoli aliongeza kuwa maono ya Mbunge ni ya muda mrefu kwani hayaangalii mahitaji ya sasa pekee bali yanazingatia manufaa ya baadaye kwa wananchi, ili Serikali iweze kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi, hususan huduma za afya.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, aliwaomba wananchi kuendelea kumuombea Mbunge wao ili aendelee kuleta maendeleo kwa kushirikiana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Comments
Post a Comment