VIJANA, WANAWAKE NA WATU WENYE ULEMAVU WAHIMIZWA KUUNDA VIKUNDI ILI KUNUFAIKA NA MIKOPO ISIYO NA RIBA


Na, Ernest Magashi

Vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wamehimizwa kuendelea kuunda vikundi na kuvisajili kisheria ili waweze kunufaika na mikopo isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya hiyo.Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi wa Kijiji cha Itunga wakati wa ziara yake ya kukabidhi vifaa vya ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho.Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Biteko aliwahimiza makundi hayo kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, inayotolewa kila mwaka kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, kwa mujibu wa sera za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.“Ninawaomba vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kuunda vikundi na kuvisajili kisheria ili muweze kuomba mikopo. Wiki iliyopita Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri alikabidhi jumla ya shilingi milioni 208 kwa vikundi 24.Serikali inaendelea kukamilisha taratibu ili kutangaza awamu nyingine ya mikopo mwezi Februari mwaka huu, na ningependa kuona vijana wa Itunga wakinufaika,” alisema Dkt. Biteko.Aliongeza kuwa lengo lake ni kuona vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wakizalisha mali, kukuza uchumi wao binafsi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa, jambo litakalowaondoa kwenye utegemezi.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, alimpongeza Mbunge kwa jitihada zake na kuwasisitiza vijana kuharakisha kuunda vikundi ili waweze kunufaika na mikopo hiyo inayotolewa na halmashauri.

Awali, Diwani wa Kata ya Bukombe, Rozaria Masokola, alisema kuwa kwa ushirikiano kati ya madiwani na watalamu wa halmashauri, vijana wataendelea kunufaika na mikopo hiyo ya maendeleo.

Comments