SHULE YA CHIEF LUASA YAPUNGUZA MSONGAMANO WA WANAFUNZI KABUHIMA


Na, Ernest Magashi

Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Chief Luasa iliyopo Kata ya Uyovu, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita umekamilika na kuanza kupokea wanafunzi mwaka huu wa masomo, hatua ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kabuhima.Akizungumza wakati wa ziara ya Diwani wa Kata ya Uyovu katika shule hiyo, Mkuu wa Shule, Zorabusa Juma, ameishukuru Serikali kwa kujenga shule yenye miundombinu bora, rafiki na wezeshi kwa wanafunzi na walimu. Amesema kuwa shule hiyo tayari imepokea wanafunzi 712 waliokuwa wakisoma Shule ya Sekondari Kabuhima.Zorabusa amesema kuwa uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya elimu umeleta mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia, hali inayochochea wanafunzi kupata elimu yenye ubora na walimu kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

“Naishukuru Serikali kwa ujenzi huu ambao umehusisha vyumba nane vya madarasa, jengo la utawala, chumba maalum cha kompyuta, maabara tatu pamoja na maktaba. Wanafunzi tayari wameanza masomo na walimu wako tayari kujituma kufikia malengo ya Serikali,” alisema Mwalimu Mkuu Zorabusa.Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Uyovu, Mathayo Kagoma, amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa mchango mkubwa alioutoa tangu hatua za awali za uanzishaji wa shule hiyo. Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 584.2 zilizowezesha kukamilika kwa mradi huo.

“Nimefika hapa kujionea ujenzi na ukamilishaji wa mradi huu ambao umeleta tija kubwa kwa kupunguza msongamano katika Shule ya Sekondari Kabuhima. Niwaombe walimu na wanafunzi kushirikiana kutunza mazingira na miundombinu ya shule,” alisema Kagoma.Diwani Kagoma ameongeza kuwa Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, ameendelea kuwa kiunganishi muhimu kati ya Kata na Serikali Kuu, hali iliyochangia kupatikana kwa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.“Dkt. Doto Biteko amekuwa kiungo muhimu katika kuwasilisha kero zetu Serikalini, jambo linalosababisha fedha kuendelea kuja. Tunamshukuru sana na tutaendelea kumuunga mkono,” ameongeza.Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kabuhima, Katabanya Paul, akizungumza kwa niaba ya wananchi, amesema kuwa wakazi wa kijiji hicho wameupokea mradi huo kwa furaha kubwa kwani usingeweza kutekelezwa kwa nguvu za wananchi wenyewe.

Amesema kuwa usikivu wa Serikali umefanikisha kusogezwa kwa huduma hiyo muhimu ya elimu karibu na wananchi, hatua inayochangia kuboresha maendeleo ya kijamii na kielimu katika eneo hilo.


Comments