SHILINGI BILIONI 6.02 KULIPA FIDIA WANANCHI 347 WALIOPISHA MRADI WA UMEME LUDEWA


Na,Ernest Magashi

Serikali inatarajia kulipa fidia kiasi cha shilingi bilioni 6.02 kwa wananchi 347 wa vijiji vya Lifua, Liugai na Masimavalafu wilayani Ludewa, mkoani Njombe, waliopisha utekelezaji wa mradi wa umeme, katika mwaka wa fedha 2026/2027.Hayo yameelezwa leo Januari 27, 2026 na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, wakati akijibu swali la Mbunge wa Ludewa, Mhe. Joseph Kamonga, katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa Pili wa Bunge la 13, kilichofanyika jijini Dodoma.Mbunge Kamonga alihoji ni lini wananchi wa Kijiji cha Liugai, Kata ya Luilo, watalipwa fidia ili kupisha utekelezaji wa mradi wa umeme katika eneo hilo.Akijibu swali hilo, Waziri Ndejembi amesema kuwa hadi kufikia Desemba 2025, zoezi la uthamini wa fidia kwa wananchi husika lilikuwa tayari limekamilika, na kwa sasa hatua iliyopo ni uhakiki wa taarifa na uwekaji wazi wa jedwali la wafidiwa kabla ya kuanza kwa malipo.Waziri Ndejembi amelihakikishia Bunge kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha zoezi la uhakiki na ulipaji wa fidia linafanyika kwa uwazi, haki na kwa wakati, ili wananchi waweze kunufaika ipasavyo na utekelezaji wa mradi huo muhimu wa nishati unaolenga kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika wilaya ya Ludewa.

Comments