Katika utekelezaji wa kauli mbiu ya “Vitongojini kama Mjini”, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wamefika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kumtambulisha mkandarasi atakayetekeleza mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 175 mkoani humo.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, ameitaka REA kumsimamia kwa karibu mkandarasi huyo ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, huku akiahidi ushirikiano kutoka Ofisi ya Mkoa.
“Nahitaji Ofisi ya Mkoa ipatiwe mpango kazi wa mkandarasi ili tuweze kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa mradi. Aidha, kwa miradi itakayokamilika, REA mtoe taarifa mapema ili izinduliwe na wananchi waanze kunufaika. Umeme ni uchumi; unachochea ajira na uwekezaji,” amesema Kanali Sawala.
Kwa upande wake, Meneja wa Usimamizi wa Miradi ya REA, Deogratius Nagu, amesema mradi huo wa kusambaza umeme ngazi ya vitongoji katika Mkoa wa Mtwara utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Januari 2026 hadi Januari 2029, na unatarajiwa kunufaisha wananchi 5,646.
Naye Meneja wa Kampuni ya Dieynem, inayotekeleza mradi huo, Novatus Lyimo, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa, huku akiahidi kutekeleza mradi huo kwa wakati na kwa kuzingatia ubora uliokubaliwa.
Na, Ernest Magashi

Comments
Post a Comment