REA KUSAMBAZA UMEME KWENYE VITONGOJI 9,009 TANZANIA BARA

Na, Ernest Magashi

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Hassan Saidy, amesema mikataba imeshasainiwa kwa ajili ya kusambaza umeme katika vitongoji 9,009 vilivyopo Tanzania Bara, hatua inayotarajiwa kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.

Saidy ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao chake na watumishi wa REA wanaohusika na usimamizi wa miradi katika mikoa mbalimbali, kilichofanyika mara baada ya kusainiwa kwa mikataba ya utekelezaji wa mradi huo.Katika kikao hicho, aliwataka Wasimamizi wa Miradi wa Mikoa kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na wadau wote wanaohusika katika maeneo ya utekelezaji wa miradi, ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa ufanisi, uwazi na kwa kuzingatia ratiba iliyopangwa.“Tarehe 17 Januari, 2026, tulisaini mikataba na wakandarasi kwa ajili ya kusambaza umeme kwenye vitongoji 9,009. Sasa tunaelekea kwenye hatua ya utekelezaji. Nimewaita hapa ili tukumbushane namna bora ya kuimarisha utendaji kazi wetu,” amesisitiza Saidy.

Ameongeza kuwa Watanzania wana matarajio makubwa kwa REA, hivyo ni wajibu wa watumishi wake kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya Serikali.“Imarisheni mawasiliano na ushirikiano na Wabunge, viongozi wa Mikoa na Wilaya, TANESCO, wakandarasi, Serikali za Vijiji na Vitongoji pamoja na wanufaika wa miradi,” ameongeza.Wakati huohuo, Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Dkt. Doto Biteko, amewaomba wananchi wa jimbo hilo kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea na taratibu za kuwafikishia umeme katika vitongoji ambavyo bado havijafikiwa.Akizungumza hivi karibuni katika ziara zake jimboni Dkt. Biteko amesema mahitaji ya umeme kwa wananchi ni makubwa, lakini Serikali kupitia REA inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha vitongoji vyote vilivyo kwenye mpango vinafikiwa.Dkt. Biteko amebainisha kuwa jumla ya vitongoji 352 wilayani Bukombe vimejumuishwa katika mpango wa kusambaziwa umeme, huku akiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Comments