Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita kwa usimamizi mzuri wa fedha na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Msangila.
Prof. Shemdoe alitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua mradi huo unaotekelezwa kwa mfumo wa Force Account, kwa gharama ya shilingi 689,901,255.00 zilizotolewa na Serikali Kuu kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia. Katika ziara hiyo, alieleza kuridhishwa na hatua ya utekelezaji wa mradi, akibainisha kuwa upo katika hali nzuri huku fedha bado zipo.
Katika pongezi zake, Prof. Shemdoe alimpongeza Mhandisi wa Ujenzi wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Haruni Fashe, kwa usimamizi makini na wenye manufaa makubwa kwa wananchi.“Nimeona kazi nzuri sana. Natarajia mradi huu utakamilika kwa wakati, kwa ubora wa hali ya juu na kuendana na thamani ya fedha iliyotolewa,” alisema Prof. Shemdoe.
Aidha, alimtakia mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha kazi inakamilika ndani ya muda uliopangwa ili kituo hicho kianze kutoa huduma kwa wananchi, kwa lengo la kufikia azma ya Serikali ya kuwaondolea wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
“Wananchi hawa wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya. Ni muhimu mkandarasi ahakikishe mradi unakamilika kwa wakati na kukabidhiwa mapema ili wananchi waanze kunufaika,” alisisitiza.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita, Grace Kingalame, akipokea pongezi hizo kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusikia kilio cha wananchi hususan wanawake, katika kuboresha huduma za afya.
“Wananchi wa Bukombe wamefurahishwa na dhamira ya Rais Dkt. Samia ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Kata ya Runzewe Magharibi kupitia ujenzi wa Kituo cha Afya Msangila,” alisema Grace Kingalame.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Runzewe Magharibi, Patrick Songolo, alimshukuru Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, kwa ushirikiano wake mzuri na madiwani pamoja na wananchi, huku akiendelea kushirikiana kwa karibu na Rais Dkt. Samia katika kuhakikisha fedha za miradi ya maendeleo zinapatikana.
“Hapo awali hatukuwa na zahanati wala kituo cha afya, achilia mbali hospitali. Huu ni mradi mkubwa sana kwetu, na tuna sababu ya kumshukuru kwa dhati Rais Dkt. Samia,” alisema Diwani Songolo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Dkt. Timotheo Masota, alisema changamoto zinazoukabili mradi ni pamoja na wazabuni kutokujitokeza kwa wakati kuomba zabuni zinazotangazwa, uhaba wa mafundi pamoja na upatikanaji wa mawe na kokoto.
Alibainisha kuwa changamoto hiyo inatokana na wananchi wengi kujikita katika shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Msasa.Dkt. Timotheo aliongeza kuwa mara baada ya kukamilika, Kituo cha Afya Msangila kinatarajiwa kuhudumia wananchi wapatao 23,906 ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipata huduma za afya katika vituo vya kata jirani.

Comments
Post a Comment