MRADI WA UMEME KUVIFIKIA VITONGOJI 352 BUKOMBE


Na, Ernest Magashi

Wananchi wa Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wametakiwa kuwa wavumilivu wakati taratibu za kufikisha huduma ya umeme kwenye vitongoji ambavyo bado havijafikiwa zikiendelea kutekelezwa, licha ya kuwa vipo kwenye mpango wa Serikali.

Wito huo umetolewa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Butinzya hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kuhamasisha maendeleo na ushiriki wa wananchi katika miradi mbalimbali ya kijamii.Dkt. Biteko alisema kuwa mahitaji ya umeme kwa wananchi ni makubwa, lakini Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na taratibu zake kuhakikisha vitongoji vyote vilivyo kwenye mpango vinafikiwa. Alibainisha kuwa jumla ya vitongoji 352 wilayani Bukombe vimejumuishwa katika mpango wa kufikishiwa umeme.

“Naomba wananchi wema wa Bukombe muendelee kuwa na subira kidogo wakati taratibu za kufikisha umeme zinaendelea. REA wako katika hatua nzuri na nina uhakika huduma hii itawafikia,” alisema Dkt. Biteko.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya kijamii, Dkt. Biteko aliwahimiza wananchi kuendelea kudumisha umoja na mshikamano kwa kujitolea nguvu zao katika miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo kusogeza mchanga, mawe na zege kwenye miradi iliyoanzishwa na wananchi, hususan ujenzi wa zahanati katika kila kijiji.

Alisema ujenzi wa zahanati katika kila kijiji utasaidia kuboresha huduma za afya na baadaye baadhi ya zahanati hizo zitapandishwa hadhi na kuwa vituo vya afya, hatua itakayopunguza changamoto za wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za rufaa.Aidha, Dkt. Biteko alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini, huku akiwaomba wananchi kuendelea kumuombea Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Butinzya, Kwizi Chenya, alimpongeza Mbunge kwa kushiriki bega kwa bega na wananchi katika shughuli za ujenzi na kuendelea kuhamasisha maendeleo katika kata hiyo.

Naye mkazi wa Butinzya, Paschal Thomas, alimshukuru Mbunge kwa kutoa ufafanuzi wa wazi kuhusu mpango wa kufikisha umeme katika vitongoji vyote, akisema wananchi wengi awali hawakuwa na ufahamu kuwa vitongoji vyao vimejumuishwa kwenye mpango huo.

Comments