KAMANDA JONGO AWAKUMBUSHA WAZAZI NA WALEZI KUIMARISHA MALEZI YA WATOTO ILI KUEPUKA MATUMIZI MABAYA YA MITANDAO YA KIJAMII


Na, Ernest Magashi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, amewakumbusha wazazi na walezi kuimarisha malezi ya watoto ili kuwalinda dhidi ya athari zinazotokana na makundi yasiyo rasmi na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ambayo yameendelea kuwa tishio kwa maadili na usalama wa watoto.

Kamanda Jongo ametoa wito huo Januari 27, 2026, katika Kijiji cha Bukandwe, Kata ya Bukandwe, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, wakati akizungumza na wananchi wa kata hiyo.Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wazazi, walezi na Jeshi la Polisi kupitia utekelezaji wa miradi ya Polisi Jamii, inayolenga kuimarisha maadili, ulinzi na usalama wa watoto pamoja na kudumisha amani katika jamii.

“Wazazi mna jukumu kubwa la kuwalea na kuwalinda watoto kwa misingi ya maadili mema ili kuwakinga dhidi ya mmomonyoko wa maadili unaochangiwa na makundi yasiyo rasmi pamoja na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii,” amesema Kamanda Jongo.Aidha, amewahimiza wananchi kuwa karibu na watoto wao, kuwapa malezi yanayozingatia maadili ya Kitanzania na Kiafrika, sambamba na kusimamia matumizi sahihi ya teknolojia na mitandao ya kijamii.

Kwa upande wake, mkazi wa Bukandwe, Mwajuma Shaban, ameishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu aliyopata kupitia mkutano huo, akisema kuwa maarifa hayo yatamsaidia kukabiliana na changamoto ya watoto kuiga mienendo mibaya kutoka mitandaoni.“Watoto wengi wanaiga vitu visivyofaa kutoka mitandao ya kijamii, hali inayopotosha maadili ya Kiafrika na utamaduni wa Kitanzania. Elimu hii itatusaidia kuwalea watoto wetu kwa uangalifu zaidi,” amesema Mwajuma.

Comments