JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA BUKOMBE YASISITIZA USIMAMIZI WA MAADILI NA UPELEKAJI WA WATOTO SHULENI
Bukombe, Geita —
Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Bukombe imeendelea kusisitiza umuhimu wa usimamizi wa maadili katika malezi ya watoto pamoja na kuhakikisha watoto wote wenye sifa wanapelekwa na kuripoti shule kwa wakati.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Bukombe, Ndg. Hassan Mohammed, wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kuzunguka kata zote 17 za wilaya hiyo ambapo leo ametembelea kata ya Runzewe Mashariki, Kata ya Igulwa na Kata ya Ushimbo.
Ziara hiyo inalenga kuimarisha mshikamano wa jumuiya, kuhamasisha wazazi na walezi kuwajibika kikamilifu katika malezi, pamoja na kusimamia kwa karibu mwenendo na maadili ya watoto wao.
Akizungumza katika ziara hiyo, Ndg. Hassan Mohammed amesema kuwa malezi bora yenye kuzingatia maadili ni msingi muhimu wa kujenga kizazi chenye nidhamu, hofu ya Mungu, uzalendo na kuwajibika kwa jamii. Ameeleza kuwa jukumu la malezi haliwezi kuachwa kwa walimu pekee, bali wazazi na walezi wana wajibu mkubwa wa kushirikiana na shule katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi sahihi.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya jitihada kubwa katika kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule na madarasa mengi katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Bukombe, jambo lililorahisisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wengi zaidi. Amesisitiza kuwa ni wajibu wa wazazi kutumia fursa hiyo kwa kuhakikisha watoto wanapelekwa shule na kunufaika na miundombinu iliyopo.
Ziara hiyo pia imetumika kuwakumbusha wazazi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika shughuli za maendeleo, kudumisha maadili ya kitamaduni na kizalendo, pamoja na kuimarisha mshikamano ndani ya Jumuiya ya Wazazi CCM kwa ustawi wa watoto na jamii kwa ujumla.
Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Bukombe imeeleza itaendelea na ziara na mikutano ya uhamasishaji ili kuhakikisha malengo ya malezi bora, elimu na maadili mema yanafikiwa katika kata zote za wilaya hiyo.
![]() |






Comments
Post a Comment