JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA BUKOMBE YAHIMIZA WAZAZI KUPELEKA WATOTO SHULE NA UFUATILIAJI WA MAADILI YA WATOTO
.
Bukombe, Geita – Januari 26, 2026:
Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bukombe, mkoani Geita, imetoa muda wa wiki moja kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wenye sifa wanaripoti shule kwa ajili ya masomo ya awali, msingi na sekondari.
Agizo hilo limetolewa leo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM wilayani Bukombe, Mohamed Hassan, wakati wa ziara ya kuhamasisha wazazi ngazi ya kata juu ya umuhimu wa elimu na uwajibikaji wa wazazi katika malezi ya watoto. Ziara hiyo pia ililenga kuwashukuru viongozi wa jumuiya hiyo ngazi ya kata kwa mchango wao wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, ulioshuhudia ushindi mkubwa wa CCM.
Akizungumza katika mikutano na Wajumbe wa Jumuiya hiyo ya Wazazi iliyofanyika kwenye vijiji na vitongoji vya kata za Busonzo, Namonge, Uyovu na Runzeweb Magharibi, Hassan aliwataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa msingi kwa kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya elimu pamoja na malezi bora yanayozingatia maadili ya Kitanzania.
Hassan alibainisha kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya wazazi kuwahusisha watoto katika shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu badala ya kwenda shule, hali aliyosema inaathiri moja kwa moja mustakabali wab watoto hao. Alisisitiza kuwa elimu ni nguzo muhimu ya maendeleo na msingi wa kuwaandaa watoto kuwa raia na viongozi bora wa baadaye.
“Tunapaswa kukaa na watoto wetu, kuwalea kwa misingi ya maadili mema na kuhakikisha wanapata elimu ili wawe viongozi bora wa kesho,” alisema Hassan
Aidha, Mwenyekiti huyo aliwataka wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa serikali na viongozi wa kuchaguliwa, akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Jimbo la Bukombe Dkt. Doto Biteko pamoja na madiwani wa wilaya hiyo, katika kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapatiwa fursa ya elimu, ikiwemo kupitia ujenzi na upanuzi wa shule unaoendelea wilayani Bukombe.
Jumuiya ya Wazazi wa CCM wilayani Bukombe imesisitiza kuwa itachukua hatua stahiki dhidi ya wazazi na walezi watakaokaidi agizo hilo, kwa lengo la kulinda haki ya mtoto ya msingi ya kupata elimu.

Comments
Post a Comment