Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita imekabidhi shilingi milioni 208 kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa vikundi 24 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiwa ni hatua ya kukuza mitaji yao na kuongeza kipato cha kiuchumi.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikopo hiyo leo Januari 2, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhadis Paskasi Muragili, amevitaka vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanairejesha kwa wakati, licha ya kutokuwa na riba.
“Tukaitumie mikopo hii kwa ufanisi zaidi ya mipango tuliyojiwekea katika shughuli za kujiinua kiuchumi. Kadri mtakavyorejesha vizuri, ndivyo mtakavyopata fursa ya mikopo mikubwa zaidi,” alisema Muragili.
Aliongeza kuwa lengo kuu la utoaji wa mikopo hiyo ni kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuwatoa katika hali ya umaskini, kuongeza kipato cha familia na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Adelina Mfikwa, aliwapongeza wanufaika wote kwa kukidhi vigezo vilivyowekwa, hatua iliyowawezesha kupata mikopo hiyo muhimu kwa maendeleo yao.Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Erick Kagoma, aliwataka wanufaika kuhakikisha wanatekeleza shughuli zao kulingana na malengo waliyoyaainisha katika mipango yao ya biashara, ili mikopo hiyo iwe chachu ya kutokomeza umaskini.
Alisisitiza kuwa mpango huu ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kujenga uchumi jumuishi na kuimarisha maisha ya wananchi kupitia uwezeshaji wa kifedha kwa makundi maalumu ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Comments
Post a Comment