Maafisa usafirishaji maarufu kama bodaboda katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wametakiwa kuendeleza umoja, mshikamano na bidii katika shughuli zao ili kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.
Wito huo umetolewa leo Januari 3, 2026 na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dkt. Doto Biteko, wakati akizungumza na maafisa usafirishaji hao katika ukumbi wa CCM wilayani Bukombe, alipofika kuwashukuru kwa kumuunga mkono na kumchagua kwa kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, pamoja na kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, madiwani.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Biteko alisema ameamua kufika kwa bodaboda kuwashukuru na kuwasikiliza, akisisitiza deni kubwa kwao kuleta maendeleo kuijenga Bukombe.
“Tushikamane kama Wanabukombe ili tuweze kuleta maendeleo. Natamani sekta ya bodaboda itambuliwe rasmi, na kila kijana aweze kuendesha chombo chake mwenyewe badala ya kulipia. Ili kufikia hilo, fanyeni kazi kwa bidii na kujiamini, msikubali kudharauliwa,” alisema Dkt. Biteko.
Aliongeza kuwa kutokana na imani kubwa waliompa wananchi kwa kumchagua, hakuna ahadi yoyote itakayoshindikana kutekelezwa, huku akieleza kuwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Biteko aliwapongeza bodaboda kwa kuwa ni miongoni mwa wachapakazi wanaoamka mapema na kulala wakiwa wa mwisho, lengo likiwa ni kupambana kuboresha maisha yao ya kila siku.
“Wapo watu kazi yao ni kukaa vijiweni, kucheza kamari au kunywa kahawa, lakini nyinyi mmechagua kufanya kazi. Hakuna mtu anayepaswa kuwadharau; badala yake mnapaswa kuheshimiwa kwa huduma mnazotoa,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri kupitia mapato ya ndani, akieleza kuwa Januari 2, 2026 Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ilikabidhi jumla ya shilingi milioni 208 kwa vikundi 24 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, huku fedha nyingine zikitarajiwa kutolewa mwezi Februari.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe, Tumbo John, aliwaomba maafisa usafirishaji kuendelea kushirikiana na Serikali pamoja na Mbunge kwa kufichua wahalifu, akibainisha kuwa bodaboda walichangia kwa kiasi kikubwa kudumisha amani na usalama wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukombe, Daniel Lutonja, aliwapongeza vijana kwa kujiajiri kupitia sekta ya usafirishaji na kuwataka kuendelea kumuunga mkono Mbunge pamoja na kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuendelea kunufaika na mipango ya Serikali.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa usafirishaji, Isaya John alimshukuru Dkt. Biteko kwa kuwakutanisha na kuwasikiliza, huku akiomba bodaboda wapatiwe ofisi ya pamoja itakayowasaidia kufanya vikao na kujadili masuala ya maendeleo yao.

Comments
Post a Comment