DKT. BITEKO AWAOMBA WANANCHI KUENDELEZA USHIRIKIANO KUJENGA BUKOMBE

Na, Ernest Magashi

Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Dkt. Doto Biteko, amewataka wananchi wa Wilaya ya Bukombe kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuijenga wilaya hiyo kwa pamoja.Wito huo umetolewa leo Januari 1,2026 wakati Dkt. Biteko alipokuwa akitoa shukrani kwa wananchi waliohudhuria sherehe za Sikukuu ya Mwaka Mpya 2026 zilizofanyika katika uwanja wa nyumbani kwake, kijiji na kata ya Bulangwa.Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Biteko alisema mwaka 2025 uliopita wananchi wa Bukombe walimpatia ushirikiano mkubwa, hususan katika ujenzi wa zahanati na miradi mingine ya maendeleo, huku Serikali ikiendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.Aliongeza kuwa uamuzi wa wananchi wa kutofanya maandamano tarehe 29 Oktoba, 2025 na kuendelea na shughuli za maendeleo ulimpa deni kubwa la kuwatumikia kwa bidii zaidi. “Nawaomba tuendelee kuchapa kazi kwa ushirikiano na umoja kwa ajili ya maendeleo ya Bukombe,” alisema Dkt. Biteko.Dkt. Biteko alisisitiza umuhimu wa mshikamano, upendo na kuwa na lugha moja ya maendeleo, akibainisha kuwa yeyote atakayejitokeza kuleta mgawanyiko hapaswi kupewa nafasi kwani Bukombe inahitaji maendeleo.Aidha, aliwashukuru wananchi kwa kukubali mwaliko wa familia yao kushiriki sherehe za Mwaka Mpya 2026, akieleza kuwa tangu mwaka 2016 familia imekuwa ikialika wananchi kusherehekea mwaka mpya nyumbani kwao, ikiwa ni mwendelezo wa utamaduni uliowekwa na wazazi wao waliotangulia mbele za haki. Awali, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhandisi Paskas Mlagili, aliwashukuru wananchi kwa kutunza amani na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali licha ya changamoto, akiwapongeza kwa kufuata maelekezo ya Serikali.Mhandisi Mlagili aliwaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Mbunge wao Dkt. Biteko, kulinda amani, kufanya kazi kwa bidii na kuongeza pato la familia na taifa, huku akibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2026 miradi mbalimbali ya maendeleo inatarajiwa kukamilika.Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed, aliishukuru familia ya Dkt. Biteko kwa kuendeleza maono ya wazazi wao ya kuwakusanya wananchi kila mwaka mpya, jambo linaloimarisha mshikamano na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo.Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasendamila, alimshukuru Mungu kwa kuwavusha wananchi kwenda mwaka mwingine na kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani, upendo na umoja.Naye Mchungaji wa Kanisa la Sabato Nyalugusu, Boniphance Kuhoka, akizungumza kwa niaba ya viongozi wa madhehebu ya dini, aliwahimiza wananchi kujikita katika kazi za uzalishaji mali na kuacha tabia ya kuwalaumu viongozi, badala yake kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.


 

Comments